POLISI WAITAKA JAMII KULEA WATOTO KWA KUZINGATIA MAADILI

Na Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Wazazi na walezi Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita, wametakiwa kuzingatia misingi ya maadili katika malezi ya watoto na kuacha tabia ya kuwaacha watoto wadogo wakizurura na kuishi mitaani kwa madai kuwa wamezoea kufanya hivyo, wakieleza kuwa hali hiyo si sahihi katika malezi.Wito huo umetolewa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Wilaya ya Bukombe, Sarafina Chamlonde, wakati wa kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya watoto katika jamii, sambamba na kufanya matendo ya huruma kwa kukabidhi misaada mbalimbali kwa wahitaji wanaohudumiwa na taasisi ya Marezi Rafiki Foundation-Bukombe.Taasisi hiyo inajihusisha na kuwalea na kuwasaidia watu wenye ulemavu, wajane na watoto yatima.Chamlonde alisema jamii ina jukumu kubwa la kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto ili kuwajenga katika misingi ya maadili, uzalendo na uwajibikaji wanapokuwa watu wazima.Alisema ukatili una sura mbalimbali, ambapo wanawake wanaweza kufanyiwa ukatili, lakini pia wanaume nao wanaweza kuwa waathirika wa vitendo hivyo, ikiwemo kunyimwa haki zao za kimahusiano.

Alitaja makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kufanyiwa ukatili kuwa ni watoto, watu wenye ulemavu na wazee.Alisema Mtandao wa Polisi Wanawake Wilaya ya Bukombe, unaoongozwa na yeye, umekuwa ukitoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kupinga ukatili wa aina mbalimbali.

 Kwa ngazi ya mkoa, mtandao huo unaongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo.

Alifafanua kuwa elimu inayotolewa inahusu ukatili wa kiuchumi, kingono, kubakwa, kulawitiwa na aina nyingine za ukatili, huku akibainisha kuwa baadhi ya mabinti wanapokwenda kutafuta ajira hukutana na vitendo vya ukatili kutoka kwa watu wanaowaahidi kuwapatia kazi.Aidha, alisema katika kipindi cha siku 16 za kampeni ya kupinga ukatili, Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu kwa jamii na kujenga uhusiano mzuri na wananchi ili waweze kutoa taarifa za uhalifu na matukio ya ukatili kwa wakati.

Alisema ushirikiano kati ya polisi na wananchi ni muhimu katika kupambana na uhalifu na kujenga jamii salama.

Chamlonde alionya kuwa baadhi ya watoto walio chini ya umri wa miaka 15 wamekuwa wakibakwa, huku wavulana wengine wakifanyiwa vitendo vya kulawitiwa. Alisema hali hiyo inahitaji juhudi za pamoja za wazazi, walezi na jamii katika kusimamia malezi ya watoto.

Alisema Jeshi la Polisi limekuwa likipokea kesi nyingi zinazohusiana na ukatili dhidi ya watoto, wakiwemo wanaoenda kufanya kazi za ndani na kukumbana na vitendo vya unyanyasaji.Aliwataka wazazi na walezi kufuatilia mienendo ya watoto wao, kuwapa malezi bora na kuchukua hatua mapema wanapoona dalili za tabia zisizofaa.

Pia alizungumzia umuhimu wa jamii kuzingatia maadili ya Kitanzania na kukemea vitendo vinavyokiuka sheria na maadili ya jamii.

Aidha, aliwaomba wananchi kuliombea Jeshi la Polisi na kuendelea kushirikiana nalo katika kuimarisha ulinzi na usalama, kupambana na uhalifu na kufichua wahalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Alisema mtu anapochukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahaka manifest na gerezani, hatua hiyo inaweza kuwa fundisho kwa wengine na kuwafanya waache vitendo vya uhalifu.

“Maandiko Matakatifu yanaeleza kuwa Mungu hapendi uovu. Hata sisi Jeshi la Polisi hatutaki uovu, ikiwemo vitendo vya ukatili vinavyofanyika katika jamii,” alisema Chamlonde.

Alitaja baadhi ya matukio ya ukatili yanayofanywa na wazazi na walezi kuwa ni pamoja na kuwaadhibu watoto kwa kuwachoma moto mikononi kwa tuhuma za kuiba fedha, akitoa mfano wa mtoto aliyechomwa moto kwa kuiba shilingi 500.

Alisema pia kumekuwa na kundi la watoto wanaoishi mitaani, ambao wanapochukuliwa na polisi na wazazi wao kuitwa kwa maelezo, baadhi yao hueleza kuwa watoto hao wamezoea kuishi mitaani na wanaporudishwa nyumbani huendelea na tabia hiyo.Aliongeza kuwa baadhi ya vijana wakiwemo wasichana wamekuwa wakitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kurekodi na kusambaza video zisizofaa, huku wengine wakijihusisha na matumizi ya bangi.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kulea watoto kwa kuzingatia mila, desturi na maadili mema ya Kitanzania badala ya kuwaacha watoto wajilee wenyewe.

Akizungumzia msaada uliotolewa kwa wahitaji, Chamlonde alisema askari wanawake walichangishana fedha kutoka katika mishahara yao ili kupata kiasi walichoweza na kukitumia kununua mahitaji kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji.Aliahidi kuwa mtandao huo utaendelea kutembelea makundi hayo na kutoa misaada pale watakapokuwa na uwezo, huku akieleza kuwa kampeni ya kutoa elimu ya kupinga ukatili itaendelea hadi Desemba 10, 2026.

Kampeni hiyo ina kaulimbiu isemayo: “Tuungane Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto: Jenga Taifa Imara lenye Haki na Usawa Kuelekea Dira 2050.”Pia aliwaomba viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kuhubiri amani, upendo na maadili mema, huku akisisitiza kuwa jamii inapaswa kusikiliza na kuheshimu ushauri wa wazazi, walezi na viongozi wa dini.

Alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kwa mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uhalifu kwa mujibu wa sheria.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa za matukio ya ukatili na uhalifu kupitia vituo vya polisi na polisi jamii vilivyopo katika kata zao, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kujikita katika shughuli za maendeleo badala ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu.Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Marezi Rafiki Foundation, Yasin Omary, alisema kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi ni cha kuigwa na watu wengine katika jamii, huku akiwataka askari hao wasiache kuwakumbuka na kuwasaidia wahitaji.Naye Mhasibu wa Marezi Rafiki Foundation, Lucy Benjamin, alilipongeza Jeshi la Polisi kupitia Mtandao wa Polisi Wanawake kwa kutoa elimu ya kupinga ukatili, akisema taasisi hiyo itahakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.Alisema pia taasisi itaendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika kila inapobaini matukio ya ukatili katika jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Marezi Rafiki Foundation, Frank Kaare, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa matendo ya huruma waliyoyafanya kwa kuwapatia wahitaji misaada mbalimbali, ikiwemo mchele, sukari, sabuni na mahitaji mengine ya watoto.Kaare alisema misaada hiyo imepokelewa kwa furaha na taasisi itahakikisha inawafikia walengwa waliokusudiwa.

Aliwaomba wadau wengine kuiga mfano huo wa Jeshi la Polisi kwa kujitolea kuwasaidia watu wenye uhitaji, akisema matendo hayo ya huruma yana thamani kubwa katika jamii na ni sehemu ya upendo kwa watu wengine.

Comments