M/K CHAMMATA TAIFA ATEMBELEA SOKO LA DHAHABU MSASA


Na, Ernest Magashi

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (CHAMMATA), Jeremia Simon, amewataka wachimbaji wa dhahabu nchini kuendelea kutumia masoko ya dhahabu yanayotambulika kisheria ili kuhakikisha usalama wa biashara zao na kupata thamani halisi ya madini wanayozalisha.Wito huo ameutoa wakati wa ziara yake ya kikazi katika Soko la Dhahabu Msasa, ambapo alikutana na kusikiliza kero na changamoto za wanachama wanaosimamia masoko ya ununuzi wa madini ya dhahabu Masumbwe na Ushirombo.Simon alisema Serikali imefanya jambo kubwa kwa kusogeza huduma ya soko la dhahabu kupitia Tume ya Madini, hatua iliyowasaidia wachimbaji kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta masoko ya dhahabu. Aliongeza kuwa juhudi hizo zinastahili pongezi kwani zimeimarisha biashara halali na kuongeza mapato ya Serikali.Katika ziara hiyo, Mwenyekiti huyo wa CHAMMATA Taifa aliitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaonunua dhahabu bila kuwa na leseni ya udalali (broker), akibainisha kuwa vitendo hivyo husababisha biashara haramu na kudhoofisha masoko rasmi ya madini.Akiwa katika Mgodi wa Msasa Gold Mine, Simon aliwapongeza wakurugenzi na viongozi wa mgodi huo kwa kuendelea kuhamasisha wachimbaji kutumia soko la dhahabu, jambo ambalo limechangia kuendelea kuwepo kwa amani na mshikamano miongoni mwa wachimbaji zaidi ya Elf 50, huku kila mmoja akifanya shughuli zake kwa kuzingatia sheria na taratibu za mgodi.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHAMMATA Wilaya ya Bukombe, Daniel Lushinge, aliipongeza ofisi ya kitaifa ya CHAMMATA kwa kuwatembelea wanachama wake wilayani humo na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili, baadhi tayari zimewasilishwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya utatuzi.Naye Meneja wa Msasa Gold Mine, Kessy Maira, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa mgodi huo, aliishukuru Serikali kwa kuwasogezea soko la dhahabu Msasa, akisema hatua hiyo imewaondolea wachimbaji adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda Ushirombo au Geita kwa ajili ya kuuza madini yao.Maira aliwaomba viongozi wa CHAMMATA kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini, ili waendelee kuuza dhahabu yao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali.


Comments