VIONGOZI WA MAIGA FOUNDATION-TANZANIA WACHANGIA BENKI YA DAMU BUKOMBE

Na, Ernest Magashi

ebukombesasablogspot.com.tz

Uongozi wa Maiga Foundation-Tanzania Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, kwa kushirikiana na wanachama na wajumbe wake, umefika katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuchangia damu katika Benki ya Damu, kutoa zawadi kwa akinamama waliojifungua pamoja na kufanya usafi wa mazingira ya hospitali hiyo.Akizungumza baada ya zoezi hilo, Katibu Mkuu Mtendaji wa Maiga Foundation-Tanzania, Joseph Maiga, alisema wamefika hospitalini hapo kwa lengo la kufanya mambo matatu makuu ambayo ni kutoa misaada mbalimbali kwa wahitaji, kufanya usafi wa mazingira na kuchangia damu.Maiga alisema miongoni mwa misaada iliyotolewa ni pamoja na sabuni kwa ajili ya wodi ya wazazi, huku akisisitiza kuwa kuchangia damu ni sehemu muhimu ya matendo ya huruma kwa jamii kwa kuwa damu hiyo inaweza kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.“Tumefika hapa pamoja na wanachama na wajumbe wetu kufanya mambo matatu. Kwanza ni kufanya matendo ya huruma kwa kutoa misaada mbalimbali, ikiwemo sabuni katika wodi ya wazazi; pili ni kufanya usafi wa mazingira ya hospitali na tatu ni kuchangia damu katika Benki ya Damu ya hospitali,” alisema Maiga.

Aidha, Maiga aliwaomba wadau wa maendeleo, wakiwemo mashirika na taasisi binafsi, kuendelea kutoa ushirikiano na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii katika taasisi za Serikali, ikiwemo kuchangia damu.Alisema pia wadau wa maendeleo wanapaswa kuyathamini makundi yenye uhitaji katika jamii kwa kuwapatia elimu ya kiuchumi pamoja na mikopo itakayowawezesha kuongeza mitaji na kuinua maisha yao.Maiga alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuwaletea wananchi maendeleo. 

Pia aliwapongeza viongozi wa Serikali kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Bukombe kupitia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akisisitiza umuhimu wa kuwafikia wenye uhitaji, Maiga alisema mashirika na wadau wa maendeleo wanapaswa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwasaidia watu wenye mazingira magumu, wakiwemo wajane, watu wenye ulemavu na watoto yatima.Alisema Maiga Foundation-Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za kijamii na kuwafikia watu wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali.Kwa upande wake, Muuguzi Rahel Reginald Uronu, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe, alisema damu iliyochangiwa na viongozi na wanachama wa Maiga Foundation-Tanzania itasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wanaohitaji kuongezewa damu.Uronu alisema hospitali hupokea wagonjwa mbalimbali wanaohitaji damu, hususan akinamama wajawazito na wanaojifungua, pamoja na watu wanaopata ajali.“Tunawashukuru Maiga Foundation-Tanzania na wanachama wao kwa kujitolea na kufanya matendo ya huruma. Kuchangia damu ni jambo kubwa kwa sababu wamegusa maisha ya wagonjwa wanaopungukiwa damu, hususan akinamama wajawazito na wanaojifungua pamoja na Watanzania wanaopata ajali,” alisema Uronu.

Naye Mteknolojia Maabara wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe, John Mariko, aliipongeza Maiga Foundation-Tanzania kwa kufika hospitalini hapo na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuchangia damu.Mariko alisema kuchangia damu ni sadaka kubwa kwa wagonjwa na kwamba damu hiyo itasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wanaofikishwa hospitalini wakiwa katika hali ya kuhitaji kuongezewa damu, wakiwemo waathirika wa ajali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maiga Foundation-Tanzania Wilaya ya Bukombe, Frank Kaare, alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na jamii na kufika hospitalini kutoa msaada kwa wagonjwa na makundi mengine yenye uhitaji.Kaare alisema kuchangia damu ni sehemu ya kutekeleza wajibu wa kijamii na ni miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa na Maiga Foundation-Tanzania katika kuwahudumia wananchi.

Alisema shirika hilo litaendelea kutafuta maeneo mbalimbali yenye uhitaji ili kutoa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi na kuunga mkono juhudi za Serikali katika utoaji wa huduma za kijamii.

Comments