WALIMU BUKOMBE WAFURAHIA MKESHA WAO NA WASANII


Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

WALIMU zaidi ya 2,000 pamoja na mamia ya wananchi wilayani Bukombe, mkoani Geita, wameungana kusherehekea Siku ya Mwalimu Duniani kwa kushiriki mkesha wa burudani uliojaa muziki, dansi na vicheko kutoka kwa wasanii mbalimbali wa muziki wa Tanzania.Mkesha huo uliofanyika Oktoba 9, 2026, uliwakutanisha walimu kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani humo, ambao walipata fursa ya kupumzika, kufurahia na kushirikiana nje ya mazingira yao ya kawaida ya kazi.

Wasanii waliotoa burudani katika mkesha huo ni pamoja na Juma Nature, Nandy, Chege, 20 Percent na Brother K, ambao walihakikisha walimu na wananchi waliohudhuria wanapata burudani ya kutosha.

Tukio hilo ni sehemu ya utaratibu wa kuwakutanisha walimu na kuwawezesha kusherehekea siku yao kwa pamoja, ulioanzishwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kushirikiana na wadau wengine.Katika mkesha huo, msanii Juma Nature aliwavutia walimu kwa kuimba nyimbo zake mbalimbali zilizowafanya wengi kusimama, kucheza na kuimba pamoja naye.Miongoni mwa nyimbo alizowaburudisha nazo ni Siku ya Kwanza Kukutana Nae, huku akiwakumbusha mashabiki wake nyimbo nyingine zilizompa umaarufu katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva.Kwa upande wake, Brother K alichangamsha mkesha huo kwa vituko na ucheshi wake, ikiwemo kutembea kwa mtindo wa kuchekesha na kuanguka, hali iliyosababisha vicheko na shangwe kutoka kwa walimu na wananchi.Hata hivyo, kilichozidisha shangwe ni kauli yake aliposema kuwa Mbunge wa Bukombe, Dkt. Doto Biteko, ni mpangaji wake.Akifafanua kauli hiyo, Brother K alisema kuwa Dkt. Biteko si mpangaji wa nyumba, bali ni mpangaji wa mipango yake kauli iliyopokelewa kwa shangwe na vicheko na kuongeza uchangamfu katika mkesha huo.Burudani za wasanii wengine, wakiwemo Nandy, Chege na 20 Percent, ziliendelea kuwafanya walimu na wananchi kushiriki kwa pamoja katika nyimbo na dansi, huku wengi wakionyesha kufurahia nafasi hiyo ya kukutana na kuburudika.Baadhi ya walimu waliohudhuria walieleza kufurahishwa na utaratibu huo wa kila mwaka, wakisema umekuwa fursa muhimu ya kuwakutanisha, kuimarisha mshikamano wao na kuwapa nafasi ya kufurahia siku yao baada ya kutekeleza majukumu ya kufundisha wanafunzi.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo, Dkt. Biteko alisema kuwa kamati ya maandalizi ilisimamia shughuli mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha walimu wanapata nafasi ya kufurahia siku yao mchana na usiku.Alisisitiza umuhimu wa kutambua mchango wa walimu katika jamii, akitumia kauli mbiu isemayo, “Mwalimu ndiyo elimu yetu.”

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, aliwapongeza walimu wa Bukombe kwa juhudi zao katika kutekeleza majukumu ya ufundishaji na malezi ya wanafunzi.Profesa Shemdoe pia alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuanzisha utaratibu wa kuwaunganisha walimu kupitia maadhimisho yao na kuwaandalia burudani zinazowawezesha kupumzika na kufurahia siku yao.Maadhimisho hayo yaliunganisha shughuli za kutambua mchango wa walimu katika elimu na burudani zilizowapa nafasi ya kusherehekea kwa pamoja, huku ujumbe mkuu ukiwa ni kuendelea kuthamini na kuunga mkono kazi ya walimu katika kujenga taifa.

Comments