MGODI WA MSASA WAAZA KUTOA HUDUMA YA KWANZA KWA WAGONJWA

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Mgodi wa Msasa Gold Mine umeanza kutoa huduma za kwanza kwa wagonjwa wanaopata changamoto za kiafya wakiwa mgodini hapo kabla ya kuwapatia rufaa kwenda katika vituo vya afya na hospitali kwa uchunguzi na matibabu zaidi.Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Msasa Gold Mine, Cosmas Bongo, wakati akizungumzia namna mgodi huo ulivyojipanga kuboresha mazingira ya usalama kwa wachimbaji wadogo wadogo wanaofanya shughuli zao katika mgodi huo.

Bongo alisema kuwa hivi karibuni mgodi umetenga eneo na kuweka chumba maalumu kwa ajili ya wataalamu wa afya kuhudumia wagonjwa, ambao watakuwa wakipatiwa huduma ya kwanza wanapopata ajali au changamoto za kiafya wakiwa kwenye shughuli za uchimbaji chini ya ardhi kabla ya kupewa rufaa.Alisema kuwa katika kuboresha huduma hizo, mgodi umenunua gari maalumu la kubebea wagonjwa, huku huduma zote zikitolewa bure hadi katika hospitali za rufaa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato na Bugando jijini Mwanza, bila mgonjwa kutozwa hata shilingi 100, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya mgodi huo ya kutoa huduma kwa jamii.

Akielezea namna huduma hiyo ya kwanza inavyosaidia wagonjwa mgodini hapo, Mganga Mkuu anayesimamia huduma za afya katika mgodi huo, Dkt. Godwin H. Otieno, alisema lengo la kuanzishwa kwa huduma hiyo ni kuwasaidia wachimbaji na watu wengine wanapopata changamoto za kiafya za ghafla wakati wa kutekeleza majukumu yao mgodini.Dkt. Otieno alisema kuwa baada ya kuwapatia wagonjwa huduma ya kwanza, huwaandalia rufaa kwenda Kituo cha Afya Uyovu, Hospitali ya Charles Kulwa na Hospitali ya Kanda ya Chato, hadi Hospitali ya Rufaa Bugando kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.

Alisema kuwa wagonjwa wenye changamoto kubwa za kiafya, hususan wanaopata ajali za kuangukiwa na mawe au vifaa ndani ya maduara, wamekuwa wakipatiwa huduma hiyo.Aliongeza kuwa tangu mwezi uliopita, walipokea mgonjwa mmoja aliyekuwa amevunjika mbavu na kumpatia huduma ya kwanza kabla ya kumkimbiza Hospitali ya Bugando, ambako baada ya kufanyiwa upasuaji ilibainika kuwa alikuwa amevunjika mbavu sita.

Hata hivyo, alisema mgonjwa huyo amepona na kurejea mgodini, ambako anaendelea na majukumu yake.Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Msasa Gold Mine, James Nkamba, maarufu kama Ng'wanakamba, alisema hatua zinazochukuliwa na uongozi wa mgodi kuanzisha huduma za kwanza kwa wagonjwa ni jambo jema na lenye umuhimu mkubwa kwa wachimbaji.

Nkamba alisema kuwa mbali na utoaji wa huduma za kwanza, uongozi wa mgodi unaendelea kuimarisha usalama kwa kujenga mitaro ya kusafirisha maji na mgodi umefikiwa na huduma ya umeme, hatua ambazo ni sehemu ya kuboresha mazingira ya uchimbaji na usalama wa wachimbaji.Naye Hepynes Elias aliupongeza uongozi wa mgodi kwa kuwajali wachimbaji wadogo wadogo kwa kuboresha mazingira yao ya kazi, kuwapatia huduma za kwanza wanapopata changamoto za kiafya pamoja na kuhakikisha mgodi unafikiwa na nishati ya umeme.

Comments