Na, Ernest Magashi
emagashi@bukombesasablog.com.
Madhehebu ya dini na taasisi zisizo za kiserikali zimetakiwa kuendelea kuwajali na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu katika jamii kwa kuwapatia mahitaji muhimu yanayoweza kuboresha maisha yao.
Wito huo umetolewa na Mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, Tawi la Igulwa, Doto Yohana Luneke, wakati wa ibada maalumu ya Sabato ya Wageni iliyofanyika Novemba 7, 2026.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na wageni mbalimbali, wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu, watu wenye ulemavu wa viungo, wajane pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupitia taasisi ya Maiga Foundation Tanzania.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mchungaji Doto alisema kanisa limeguswa na mahitaji ya watu hao na kutoa msaada wa vitu mbalimbali, zikiwemo sabuni pamoja na vitabu kwa ajili ya kujifunza.
"Leo ni siku yetu ya furaha na ni sehemu ya Sabato njema. Hata Yesu alitumia siku ya Sabato kutenda mema. Namshukuru sana Mungu kwa kutuwezesha kujumuika katika ibada hii. Kanisa limeguswa na kutoa msaada huu licha ya kuwa ni sehemu ya utaratibu wa kanisa letu," alisema Mchungaji Doto.
Aliwaomba waumini kutambua kuwa kwenda kanisani siyo kwa ajili ya kusali pekee, bali pia ni kuhakikisha wanawagusa na kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali katika jamii.
Alisema kama Yesu alivyowagusa na kuwasaidia vipofu, viziwi na watu wengine wenye mahitaji, waumini wanapaswa kuiga mfano huo kwa kuwasaidia wengine ni sehemu ya ibada yenye baraka.
Kwa upande wake, muumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Igulwa, Ellen John, alimshukuru mchungaji wao kwa kuwa na maono ya kuwajali watu wenye uhitaji, akisema amebarikiwa na ibada hiyo kutokana na kuona watu wenye mahitaji wakikumbukwa na kusaidiwa.
Ellen pia aliwashukuru viongozi wa taasisi ya Maiga Foundation kwa juhudi zao za kuwajali watu wenye mahitaji na kutoa wito kwa makanisa mengine kuiga mfano huo kwa kuwasaidia wenye uhitaji.
Aidha, alihimiza jamii kuendelea kuwakubali na kuwathamini watu wenye ulemavu, badala ya kuwabagua, huku akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Naye Neema Bulegi alisema amefurahishwa na ibada hiyo ya Sabato kwa kupata nafasi ya kusali pamoja na watu wenye mahitaji mbalimbali, akieleza kuwa mchungaji ameonesha mfano wa upendo kwa kuwajali watu hao.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mchungaji wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, Mtaa wa Bukombe, Philipo Nimrod, aliwaomba wazazi na walezi kuendelea kuwatunza watoto na kuwafundisha maadili ya kimungu.
Alisisitiza kuwa watoto wanapaswa kuwaheshimu na kuwasikiliza wazazi pamoja na viongozi wa dini ili wakue katika hekima na kimo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Maiga Foundation Wilaya ya Bukombe, Frank Kaare, alitoa shukrani kwa kanisa kwa niaba ya taasisi hiyo kutokana na kuwafikia na kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali.
Kaare alisema Mchungaji Doto Yohana Luneke ni miongoni mwa watu waliowahi kuonesha moyo wa kujitolea kwa kusaidia watoto watano pamoja na watu wengine wenye uhitaji kwa kuwafikia hadi majumbani mwao.
Alisema Mchungaji Doto ana moyo wa huruma na upendo unaowafanya watu wenye mahitaji wajisikie faraja, huku akiliomba kanisa kuendelea kudumisha moyo huo wa kuwasaidia wengine kama ilivyosisitizwa katika ujumbe wa mchungaji huyo.

Comments
Post a Comment