MAREZI RAFIKI FOUNDATION YAKABIDHI MSAADA KWA WAHITAJI ULIOTOLEWA NA POLISI BUKOMBE

Na Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Viongozi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Marezi Rafiki Foundation wilayani Bukombe, mkoani Geita, wamekabidhi misaada mbalimbali iliyotolewa na Mtandao wa Polisi Wanawake Wilaya ya Bukombe kwa makundi ya watu wenye uhitaji wanaohudumiwa na taasisi hiyo.Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, mlezi wa makundi ya wahitaji yanayohudumiwa na Marezi Rafiki Foundation, Sada Ramadhan, alisema kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi cha kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu ni cha kuigwa na jamii pamoja na wadau wengine.Ramadhan alisema matendo ya huruma kwa watu wenye uhitaji ni jambo linalompendeza Mungu, akieleza kuwa watu wanaojitoa kuwasaidia wengine wanapaswa kuungwa mkono ili kuendelea kuwafikia wahitaji zaidi.Aliongeza kuwa jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kusaidiana na kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye mazingira magumu.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Marezi Rafiki Foundation, Frank Kaare, alisema amefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Mtandao wa Polisi Wanawake wa Bukombe ya kutembelea na kuwasaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji.Kaare alisema misaada hiyo imekabidhiwa kwa makundi yanayotambuliwa na taasisi hiyo, wanawake wajane, watu wenye ulemavu, watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.Alilishukuru Jeshi la Polisi kwa moyo wa kujitolea na misaada iliyotolewa, ikiwemo mchele, sukari, sabuni pamoja na mahitaji mbalimbali ya watoto.Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu wajibu wa kutoa taarifa za uhalifu, hususan vitendo vya ukatili vinavyofanywa dhidi ya wanawake na watoto.Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi Wilaya ya Bukombe, Sarafina Chamlonde, alisema Mtandao wa Polisi Wanawake umeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kupinga ukatili wa aina mbalimbali, sambamba na kufanya matendo ya huruma kwa kuwasaidia watu wenye uhitaji.

Chamlonde aliomba uongozi wa tasisi ya Marezi Rafiki Foundation kuongeza kundi la wagane ili kuweka usawa na uuwiano wa watu wenye  uhitaji ikiwa wanaume waneachiwa familia na wakezao baada ya kudariki duni wanahaki pia ya kuongezwa kwenye tasisi.Alisema jamii ina jukumu kubwa la kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto ili kuwajenga katika misingi ya maadili, uzalendo na uwajibikaji watakapokuwa watu wazima.

Alieleza kuwa mtandao huo utaendelea kutembelea makundi mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya kutoa elimu na misaada kulingana na uwezo utakaokuwepo, huku akibainisha kuwa kampeni ya kutoa elimu ya kupinga ukatili itaendelea hadi Desemba 10, 2026.Kampeni hiyo ina kaulimbiu isemayo: “Tuungane Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto: Jenga Taifa Imara lenye Haki na Usawa Kuelekea Dira 2050.”Alisema Mtandao wa Polisi Wanawake Wilaya ya Bukombe, unaoongozwa naye, umekuwa ukitoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kutambua, kuripoti na kupinga vitendo vya ukatili wa aina mbalimbali.Kwa ngazi ya Mkoa wa Geita, mtandao huo unaongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo.

Comments