Na, Ernest Magashi
emagashi@bukombesasablog.com.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuendelea kusukuma maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Erick Kagoma, wakati akihitimisha kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika wiki iliyopita.
Kagoma alisema kuwa Dkt. Biteko, awepo au asiwepo kwenye vikao vya baraza, amekuwa akifuatilia na kupata taarifa za maendeleo ya halmashauri kutokana na juhudi kubwa anazozifanya za kusukuma upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema mbunge huyo amekuwa akionesha kujali maendeleo ya wananchi na kufahamu kinachoendelea katika vikao vya baraza, jambo linalostahili pongezi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskasi Mragili, aliwataka madiwani kuendelea kushirikiana na wataalamu wa halmashauri katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku wakidumisha kaulimbiu ya mbunge huyo ya Kusema na Kutenda.
Hatua hiyo ya pongezi imekuja wakati Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ikitangaza kupokea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza mwanzoni mwa wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, alisema halmashauri hiyo imepokea jumla ya shilingi 1,527,055,260 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mfikwa alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi milioni 30 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha Maabara ya Biolojia katika Shule ya Sekondari Lyambamgingo, huku kiasi kingine cha shilingi milioni 30 kikielekezwa katika kukamilisha maabara ya Shule ya Sekondari Msonga.
Alisema pia shilingi milioni 90 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Bulega, huku shilingi bilioni 1,327,055,260 zikielekezwa katika ujenzi wa mradi wa Soko Kuu la Ushirombo.
Aidha, Mfikwa alisema halmashauri imepokea shilingi milioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Zahanati ya Ishololo na shilingi milioni 15 nyingine kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Zahanati ya Nalusunguti na shilingi milioni 20 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba zahanati ya Kiziba.

Comments
Post a Comment