MADIWANI WAMEAZIMIA KUTUNGA SHERIA NDOGO KUDHIBITI MMOMONYOKO WA MAADILI KWA WATOTO

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameazimia kuanzisha mchakato wa kutunga sheria ndogo itakayosaidia kudhibiti mmomonyoko wa maadili kwa watoto, huku wazazi wakibebeshwa wajibu wa kuwajibika pale watoto wao wanapokiuka taratibu za malezi na makuzi.Hoja hiyo iliibuliwa na madiwani mbalimbali wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichojadili maazimio ya Kamati ya Kudhibiti UKIMWI (CMAC).

Akichangia hoja hiyo, Diwani wa Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma, alisema hali ya mmomonyoko wa maadili katika Mji Mdogo wa Uyovu imekuwa ikizidi kuongezeka, akieleza kuwa kila siku nyakati za jioni hukutana na makundi ya watoto zaidi ya 100 ambao hawana sehemu maalumu za kulala.Alisema hali hiyo inachangia kujenga kizazi ambacho kinaweza kukumbwa na changamoto kubwa za kitabia endapo hatua za mapema hazitachukuliwa.

Kagoma aliitaka halmashauri kuandaa sheria ndogo itakayodhibiti hali hiyo na kuwawajibisha wazazi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

Alisema kwa sasa watoto wanapokamatwa na polisi mara nyingi huachiwa kutokana na umri wao kuwa chini ya miaka 18, huku kukiwa na changamoto ya kupata mahali pa kuwaweka tofauti na watu wazima.Alisema sheria hiyo itasaidia kuweka utaratibu wa kuwawajibisha wazazi na kuchukua hatua zinazolenga kuwalinda watoto dhidi ya mazingira hatarishi.

Aidha, alisema baadhi ya shule zimekuwa zikichangia mmomonyoko wa maadili, akitolea mfano matukio ya hivi karibuni ambapo baadhi ya wanafunzi walizua taharuki kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuhitimu kidato cha nne nje na Bukombe.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Iyogelo, Juma Lushiku, aliunga mkono hoja hiyo na kuitaka menejimenti ya halmashauri kuhakikisha walimu wanasimamia maandalizi ya sherehe za wanafunzi shuleni ili kuzuia matumizi ya nyimbo zisizozingatia maadili.

Alisema pia ni muhimu kufuatilia mienendo ya wanafunzi ili kubaini iwapo baadhi yao wamekuwa wakitoka nje ya shule na kujifunza vitendo vinavyoweza kuchangia mmomonyoko wa maadili.Naye Diwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Chenya, alisema kutungwa kwa sheria ya kudhibiti mienendo ya watoto ni jambo muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Diwani wa Viti Maalumu, Jenipha Makemo, aliunga mkono wazo la kutungwa kwa sheria hiyo na kuiomba Serikali kurejesha matumizi ya viboko shuleni kama mojawapo ya njia za kudhibiti mmomonyoko wa maadili.Makemo alisema matumizi yasiyofaa ya simu za mkononi pamoja na kuiga tamaduni za kigeni kupitia mitandao ya kijamii ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuathiri mwenendo wa wanafunzi.

"Kinachoendelea ni kibaya sana. Naomba sheria itungwe. Ni aibu mwanafunzi anamiliki simu na badala ya kutumia vizuri, mtoto akikutwa na simu mzazi achukuliwe hatua. Wanafunzi wanaiga tamaduni za kigeni kupitia simu," alisema Makemo.Diwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga, alisema hali ya maadili kwa watoto kwa sasa inahitaji uangalizi wa karibu, akieleza kuwa baadhi ya watoto wamekuwa wakijihusisha na biashara ndogondogo za kuuza mayai na karanga katika kumbi za starehe, hasa nyakati za usiku.

Alisema hali hiyo inahitaji hatua za haraka, hivyo aliunga mkono pendekezo la kutungwa kwa sheria ndogo itakayodhibiti changamoto hiyo.Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Boniphance Shitobelo, alisema kupitia maazimio ya Kamati ya CMAC, halmashauri inapaswa kuanzisha mchakato wa kutunga sheria ndogo itakayoweka utaratibu wa kuwawajibisha wazazi wanaoshindwa kusimamia malezi ya watoto wao.

Alisema pia kuna haja ya kufuatilia vijana wanaotoka maeneo mbalimbali na kuishi katika maeneo ya halmashauri ili kubaini wanapoishi na watu wanaowasimamia.Aliongeza kuwa walimu wanapaswa kufuatilia wanafunzi kuanzia darasa la saba hadi sekondari wanaomiliki simu za mkononi na kuzitumia kwa mawasiliano ya siri ambayo wazazi wao hawana taarifa nayo.

Katika maazimio ya Kamati ya CMAC ya Oktoba 10, 2026, menejimenti iliagizwa kuanzisha mchakato wa kutunga sheria ndogo ya halmashauri itakayosaidia kuzuia watoto wadogo kutembea au kuzurura nyakati za usiku ili kupunguza matukio ya ukatili.Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Mlingwa Methusela, aliwaomba madiwani kuzingatia sheria iliyopo badala ya kukimbilia kutunga sheria nyingine inayohusu watoto.

Alisema Sheria ya Mtoto, Sura ya 13, Toleo la mwaka 2023, ndiyo sheria mama inayosimamia masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi na ustawi wa mtoto.

Alisema ni muhimu kwa madiwani na wadau wengine kushirikiana katika kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo, ambayo tayari imeweka bayana wajibu wa wazazi katika kumlea na kumlinda mtoto dhidi ya mazingira yasiyofaa.Aliongeza kuwa hata kama halmashauri itatunga sheria nyingi, changamoto ya mmomonyoko wa maadili inaweza kuendelea endapo usimamizi wa sheria na malezi hautazingatiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, alisema kutungwa kwa sheria ndogo ni jambo linalowezekana, ingawa mchakato wake unaweza kuchukua muda mrefu.Aliwataka wazazi kutimiza wajibu wao wa malezi na kuhakikisha wanawafuatilia watoto wao, akisema licha ya kuwepo kwa watoto wanaozurura mitaani, kila mtoto ana mahali alipotoka na mzazi au mlezi anayepaswa kuwajibika.

Mfikwa alisema walimu wamekuwa wakisimamia wanafunzi wakati wa masomo, lakini baadhi ya wazazi wamekuwa wakishindwa kuwafuatilia watoto wao nyumbani, hasa wakati shule zinapofungwa.

Alisema wapo wazazi ambao wamekuwa wakitamani watoto wao wanapofunga shule waende sehemu nyingine badala ya kubaki nyumbani, jambo linaloweza kupunguza nafasi ya wazazi kufuatilia mienendo yao.

Aliwaomba madiwani kusimamia sheria zilizopo za halmashauri zinazokataza watoto kuzurura, hususan katika maeneo ya kumbi za starehe na sehemu nyingine zilizopigwa marufuku, ili kuhakikisha usalama na ustawi wao.Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskasi Muragili, aliwaomba madiwani kusimamia kanuni na sheria zinazoongoza uendeshaji wa vikao vyao.Aidha, aliagiza pembejeo za kilimo kufikishwa katika kila kata na wakulima kufuatwa majumbani ili kusajiliwa na kuhakikisha wananufaika na mbolea za ruzuku ya Serikali.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, aliwataka wataalamu wa halmashauri kuhakikisha maazimio yote ya Baraza la Madiwani yanatekelezwa, likiwemo pendekezo la kuanzisha mchakato wa kutunga sheria ndogo itakayosaidia kudhibiti mmomonyoko wa maadili kwa watoto.


Comments