DIWANI AHAMASISHA WANANCHI KUPOKEA MRADI WA MAJI WA SHILINGI MILIONI 300 BUTINZYA

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Wananchi wa Kata ya Butinzya, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wametakiwa kuupokea na kuulinda mradi wa maji safi na salama unaotarajiwa kutekelezwa kuanzia Kijiji cha Sinamila, kwa lengo la kuwaondolea adha ya upatikanaji wa huduma hiyo.Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Mathias Chenya, wakati wa kumtambulisha mkandarasi atakayetekeleza mradi huo kwa wananchi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Sinamila.

Kwizi alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, akisema Serikali imetoa zaidi ya Shilingi milioni 300 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo wa maji safi na salama.Alisema mradi huo, unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi huu, utakapokamilika utaondoa changamoto ya ukosefu wa maji ambayo wananchi wamekuwa wakikabiliwa muda mrefu."Serikali imeleta fedha na leo tunamtambulisha kwenu mkandarasi. Niwaombe muupokee mradi huu na kumpa ushirikiano mkandarasi, ikiwemo kutoa fursa za ajira za muda kwa vijana wetu. Mradi huu ni hatua kubwa ya maendeleo kwa wananchi wa Kata ya Butinzya," alisema Kwizi.Kwa upande wake, Afisa Mipango, Julieth Zacharia, aliwaomba wananchi kushirikiana na Serikali katika kuulinda na kuutunza mradi huo, ikiwemo kutunza mazingira yanayozunguka chanzo cha maji ili kuhakikisha huduma hiyo inaendelea kupatikana kwa muda mrefu.Mratibu Msaidizi wa Mradi huo, Dorice Kinyanga, alisema Kata ya Butinzya, hususan Kijiji cha Sinamila, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama.

Kinyanga aliwashukuru viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Sinamila kwa kushirikiana katika kuhakikisha maeneo ambayo mabomba ya maji yatapita yanapatikana bila kuwepo kwa madai ya fidia kutoka kwa wananchi.

Alisema hatua iliyofikiwa ya kumtambulisha mkandarasi inaashiria maandalizi ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo, huku akiwaomba wananchi kumpa ushirikiano ili kazi ikamilike kwa wakati uliopangwa, kuanzia Novemba 2026 hadi Mei 2027.Naye Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Bukombe, Lung'wang'wa Magulu, alisema mchakato wa upatikanaji wa mradi huo ulianza Juni 2025 na kwamba Novemba 12, 2026, mkandarasi amekabidhiwa eneo la mradi kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Alisema mradi huo unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 8,000, kuanzia Kijiji cha Sinamila, huku akieleza kuwa maeneo mengine ya kata ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo yataendelea kusubiri awamu nyingine ya utekelezaji kadiri fedha zitakavyopatikana.Akifafanua kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Magulu alisema chanzo cha maji kitakuwa Sinamila, ambapo maji yatapandishwa kwa kutumia mabomba hadi kwenye tenki litakalojengwa katika Shule ya Msingi Sinamila. Aliongeza kuwa kutakuwa na vituo vitatu vya kuchotea maji katika kijiji hicho.

Aidha, alimuagiza mkandarasi kuhakikisha anawashirikisha wazawa katika utekelezaji wa mradi huo kwa kuwapatia ajira za muda, pamoja na kutumia bidhaa na huduma zinazopatikana katika eneo husika, ikiwemo mchanga na kokoto.

Alisema wananchi watakaopata fursa za ajira wanapaswa kuwa tayari kushiriki katika kazi mbalimbali za ujenzi, huku akisisitiza kuwa kukosekana kwa nguvu kazi ya wazawa kwa wakati hakupaswi kusababisha kusimama kwa utekelezaji wa mradi.Kwa upande wake, mkandarasi wa mradi huo, Bernad Salagu, aliwaomba wananchi kushiriki katika ulinzi shirikishi wa vifaa vya mradi ili kuzuia wizi wa vifaa vya ujenzi, ikiwemo saruji, ambao unaweza kusababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wake.

Salagu alisema kampuni yake iko tayari kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia makubaliano na mpango uliowekwa, akiahidi kutowaangusha wananchi na Serikali na kwamba maandalizi ya kuanza kazi mwezi huu yamekamilika.Akizungumza katika mkutano huo, mkazi wa Kijiji cha Sinamila, Ndekele Makulilo, aliishukuru Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa eneo hilo kuhakikisha wanapata mradi huo, akisema utawasaidia wananchi, hususan wanawake, kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji

Comments