WANACHAMA WA CCM WAKUMBUSHWA KULIPA ADA ZA UANACHAMA

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekumbushwa kulipa ada za uanachama ili kuendelea kuwa wanachama hai, kuelekea uchaguzi wa ndani ya chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.Wito huo umetolewa na mkufunzi Bahati Masalu wakati akitoa semina kwa wanachama wa CCM wa Kata ya Bulega, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, iliyohusu zana za mabadiliko katika falsafa ya Chama Cha Mapinduzi na umuhimu wa kulipa ada za uanachama.Masalu aliwataka wanachama kutambua umuhimu wa kulipa ada kwa wakati, kuendelea kudumisha uzalendo kwa chama chao na kuimarisha misingi ya itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea.

Akifungua semina hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila, aliwaomba wanachama wa Kata ya Bulega na maeneo mengine mkoani humo kutumia mafunzo hayo kujiongezea uelewa kuhusu misingi, itikadi na wajibu wao ndani ya chama.Kasendamila alisema mafunzo hayo yatawajengea wanachama uwezo wa kuelewa majukumu yao na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa ndani ya chama unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.Aliongeza kuwa wanachama ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria semina hiyo kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao wanapaswa kupata fursa ya kujifunza kupitia wanachama waliohudhulia mafunzo.Kwa upande wake, katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe Leonard Mwakalukwa, alipokuwa akimkaribisha mwenyekiti huyo kufungua semina, aliwaomba wanachama kufuatilia kwa makini mada zitakazokuwa zikitolewa ili waweze kunufaika na mafunzo hayo.Naye Diwani wa Kata ya Bulega, Erick Kagoma, alimpongeza mkufunzi pamoja na wanachama waliojitokeza kushiriki mafunzo hayo licha ya kuwa na majukumu mbalimbali ya kila siku.Kagoma aliwataka wanachama kuendeleza ushirikiano na kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kujenga umoja na kuimarisha chama, akibainisha kuwa baadhi yao huenda wamesahau au hawana uelewa wa kutosha kuhusu misingi ya CCM.Aliwataka washiriki kwenda kuwafikishia wanachama wengine elimu waliyoipata ili kuongezea uelewa kuhusu misingi na taratibu za chama.

Aidha, aliwasisitiza wanachama kuzingatia mafundisho waliyopata kwa kuendeleza upendo na mshikamano ndani ya chama, huku wakithamini viongozi wao, akiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alisema amekuwa akileta fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.Akizungumzia malengo ya uhamasishaji wa wanachama, Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Bulega, Mariko Kashmi, aliahidi kusajili wanachama wapya 300 na kuwakabidhi ifikapo Oktoba 20, 2026.Kashmi alisema semina hiyo imewasaidia kujifunza na kukumbushwa mambo mbalimbali muhimu kuhusu chama, ikiwemo wajibu wa kulipa ada za uanachama ili kuendelea kuwa wanachama hai.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Bulega, Stephan Masobheji, aliwashukuru viongozi wa chama ngazi ya wilaya, mkoa na taifa kwa kuona umuhimu wa kuandaa semina hiyo kwa wanachama, akisema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa na kuimarisha chama katika ngazi ya kata.

Comments