WALIMU KESHO KUFURAHIA TENA SIKU YAO BUKOMBE

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

WALIMU wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita pamoja na wageni kutoka maeneo ya jirani kukutana tena kesho Oktoba 9, 2026, wataungana kusherehekea Siku ya Mwalimu Duniani katika maadhimisho yatakayofanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo.

Mratibu wa maadhimisho hayo, Mwalimu Abdulmajid Yusuph, amesema maandalizi yamekamilika kwa kiwango kikubwa huku kamati ikiwa imejipanga kuhakikisha walimu wanapata fursa ya kusherehekea siku yao kwa furaha, upendo na mshikamano.Yusuph amewataka walimu na wageni waalikwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki pamoja katika maadhimisho hayo, akisema yameandaliwa kwa lengo la kuwakutanisha walimu, kubadilishana uzoefu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Mwalimu Ramdhan Ng’oi, amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Wajibika Kumfanya Mwalimu Afurahi,” huku akiwataka wajumbe wa kamati kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kama zilivyopangwa.Ng’oi amesema kamati imeanza kupokea wageni mbalimbali na maandalizi ya uwanja yanaendelea, huku wajumbe wakiendelea kutekeleza majukumu yao katika maeneo mbalimbali.Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, ambaye pia ni mwalimu kwa taaluma, ameitaka kamati kuhakikisha maadhimisho hayo yanakuwa ya furaha, burudani na kumbukumbu nzuri kwa walimu watakaoshiriki.

Dkt. Biteko amesema maadhimisho hayo yamekuwa sehemu ya kuwakutanisha walimu, kujifunza na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maisha na taaluma yao.

Amesema maandalizi yanazingatia upatikanaji wa chakula, vinywaji na burudani, pamoja na shughuli mbalimbali zitakazowapa walimu nafasi ya kusherehekea siku yao kwa pamoja.Amesema walimu ni miongoni mwa makundi muhimu ya watumishi wanaotekeleza majukumu makubwa katika jamii, akieleza kuwa mchango wao katika kujenga na kuendeleza taifa unapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa.

Dkt. Biteko amesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira bora kwa walimu, akieleza kuwa kuwekeza katika mwalimu ni sehemu ya kuwekeza katika elimu na maendeleo ya taifa.

Aidha, ameitaka kamati kuhakikisha walimu wanapokelewa vizuri, ratiba inazingatiwa na shughuli zote zilizopangwa zinatekelezwa kwa wakati ili maadhimisho hayo yafanikiwe na kuwaacha washiriki na kumbukumbu nzuri.

Kwa mujibu wa ratiba, shughuli zitaanza asubuhi kwa mashindano ya kwaya kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Bukombe, ambapo mshindi atapata nafasi ya kutumbuiza mbele ya mgeni rasmi.Aidha, kutakuwa na michezo mbalimbali ikiwemo basketball, netball shootout pamoja na mchezo wa soka kati ya walimu wa Chuo cha Ualimu Katoke na timu ya Walimu wa Wilaya ya Bukombe.

Mbali na michezo, walimu watashiriki matembezi ya kuadhimisha siku hiyo, yatakayoanzia eneo la benki mjini Ushirombo na kuongozwa na brass band hadi katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo.Usiku, kutakuwa na mashindano ya rap freestyle, dancing competition pamoja na burudani nyingine zitakazolenga kuwapa walimu nafasi ya kujiburudisha na kusherehekea siku yao.

Shughuli hizo zitahitimishwa kwa Usiku wa Mwalimu, utakaokuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali akiwemo Juma Nature, Nandy, Chege, 20 Percent na Brother K.

Comments