WAJUWE WANAFUNZI SITA WALIOPATA ZAWADI SIKU YA MWALIMU DUNIANI BUKOMBE

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

WANAFUNZI sita kutoka shule za msingi na sekondari wilayani Bukombe, mkoani Geita, wamezawadiwa fedha taslimu baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya uandishi wa insha yaliyolenga kuonyesha umuhimu wa mwalimu katika jamii.

Wanafunzi hao walikabidhiwa zawadi hizo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yaliyofanyika Oktoba 9, 2026, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ushirombo wilayani Bukombe.Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, aliwataja wanafunzi hao kuwa ni miongoni mwa waliofanya vizuri katika mashindano hayo yaliyohusisha shule za msingi na sekondari.Kwa upande wa shule za msingi, washindi ni Anitha Msafiri Msigwa kutoka Shule ya Msingi Bulumbaga, aliyepata Shilingi 300,000; Angel Amos Kisandu wa Shule ya Msingi Msonga, aliyepata Shilingi 200,000; na Irene Sikitu Shija wa Shule ya Msingi Mtakuja, aliyepokea Shilingi 100,000.

Katika kundi la shule za sekondari, Mpanga Petro Kitasuka wa Shule ya Sekondari Bukombe alipata Shilingi 300,000, Shadrack Costantine Musa wa Shule ya Sekondari Uyovu alipata Shilingi 200,000, huku Adriano Mabula Ngasa wa Shule ya Sekondari Namonge akipokea Shilingi 100,000.Mashindano hayo yalianzishwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe Naibu Waziri Mkuu mstafu, Dkt. Doto Biteko, kwa lengo la kuwashirikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutafakari na kueleza umuhimu wa mwalimu katika jamii kupitia uandishi wa insha.Dkt. Biteko alisema maswali ya mashindano hayo huandaliwa kwa kuzingatia viwango vya elimu vya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuwapa fursa ya kushiriki na kuonyesha uwezo wao.Aidha, aliitaka jamii kuendelea kumheshimu na kumpa thamani mwalimu kutokana na mchango wake katika maendeleo ya elimu na jamii kwa ujumla, akisisitiza kuwa heshima hiyo inapaswa kuanzia ngazi ya mtaa, kata na wilaya hadi taifa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani Bukombe, ambaye pia ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Ikuzi, Abdulmajid Yusuph Ahmada, alisema mashindano ya mwaka 2026 yalilenga kupima uwezo wa wanafunzi kueleza umuhimu wa mwalimu katika jamii.Alisema wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walishindanishwa kwa kuzingatia makundi yao ya elimu na washindi wakapewa zawadi wakati wa maadhimisho hayo.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, aliwapongeza walimu wa Wilaya ya Bukombe kwa mafanikio yao katika sekta ya elimu.Profesa Shemdoe alisema walimu wa Bukombe wameendelea kufanya vizuri, huku akibainisha kuwa wilaya hiyo imeshika nafasi ya kwanza kimkoa kwa miaka minne na nafasi ya tisa kitaifa mwaka huu. 

Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto zinazowakabili walimu wa Bukombe ili kuboresha mazingira yao ya kazi na utoaji wa elimu.Aidha, aliwataka walimu kuhakikisha wanawatendea wanafunzi haki, kuwajali na kuwalea katika misingi ya utu wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Comments