Na, Ernest Magashi
emagashi@bukombesasablog.com.
WALIMU wa shule za msingi na sekondari Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, wamepongezwa kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na nidhamu, hali iliyochangia wilaya hiyo kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani, ikiwamo kushika nafasi ya kwanza kimkoa na nafasi ya tisa kitaifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani yaliyofanyika wilayani Bukombe na kuhudhuriwa na walimu zaidi ya 2,000.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Profesa Shemdoe aliwapongeza walimu wa Bukombe kwa kazi kubwa wanayoifanya katika sekta ya elimu, akibainisha kuwa kada ya ualimu imezalisha watumishi wengi wanaohudumia taifa katika sekta mbalimbali.
Alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kuanzisha utaratibu wa kuwaunganisha walimu kupitia maadhimisho hayo, akisema kaulimbiu yake ya Kusema na Kutenda ina ujumbe muhimu katika kuboresha sekta ya elimu.
“Nampongeza Dkt. Biteko kwa kaulimbiu yake ya Kusema na Kutenda. Huu ni ujumbe muhimu katika sekta ya elimu. Niwaombe walimu kuelekeza malengo na dhamira zenu katika kufikia mafanikio na matokeo bora kwa walimu na wanafunzi,” alisema Profesa Shemdoe.
Alisema amefahamishwa kuwa maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani katika Wilaya ya Bukombe yalianza mwaka 2018 na hufanyika kila mwaka tarehe 8 au 9 Oktoba, baada ya siku rasmi ya maadhimisho hayo duniani, Oktoba 5.
Alisema utaratibu huo ni muhimu kwa kuwa unawawezesha walimu kukutana, kutambua mchango wao katika jamii na kujifunza kutoka kwa viongozi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu.
Profesa Shemdoe aliwapongeza walimu wa Bukombe kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa kwa miaka minne na nafasi ya tisa kitaifa, akiwataka kuendelea kushirikiana ili kuboresha zaidi matokeo ya wanafunzi.
Aidha, aliahidi kuendelea kufuatilia changamoto zinazowakabili walimu wa wilaya hiyo na kuzitaka halmashauri nchini kuhakikisha zinalipa madeni ya walimu, hususani wale walioajiriwa hivi karibuni.
Kuhusu ujenzi wa Shule ya Msingi Msasa, alisema atahakikisha suala hilo linafuatiliwa ili shule hiyo ujenzi unaohitajika uanze.
Alisema Bukombe imepiga hatua kubwa katika matokeo ya elimu ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo wilaya hiyo ilikuwa ikishika nafasi za mwisho kimkoa.
Aliwataka walimu kutoridhika na mafanikio yaliyopatikana, bali kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine wa elimu ili kufikia matokeo bora zaidi kitaifa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, aliwashukuru wajumbe wa kamati ya maandalizi na wadau waliochangia kufanikisha maadhimisho hayo, akiwataja Benki ya CRDB na Jembe ni Jembe.
Alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuwafanya walimu wajisikie kuthaminiwa kwa mchango wao katika kuelimisha na kujenga taifa.
“Nilikuwa nikiwaambia wajumbe wa kamati ya maandalizi kuwa jambo moja tunalopaswa kuhakikisha ni kwamba mwalimu wa Bukombe anafurahi siku hii. Mhudumieni vizuri na hakikisheni anapata kila kitu kilichoandaliwa kwa ajili yake. "Tutakuwa na burudani za muziki na wasanii mbalimbali, na tutasherehekea kwa kauli moja kwamba mwalimu ndiyo elimu yetu. Kwa kweli, walimu nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya,” alisema Dkt. Biteko.
Alisema walimu wana jukumu kubwa zaidi ya kufundisha darasani, kwa kuwa pia huwalea wanafunzi, huwajengea tabia njema na kuwafundisha nidhamu.
Alibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi hutoka katika mazingira magumu ya kifamilia, hivyo walimu huwa sehemu muhimu ya kuwasaidia na kuwapa mwongozo wa maisha.
Akitoa mfano wa uzoefu wake alipokuwa mwalimu, Dkt. Biteko alisema aliwahi kumfuatilia mwanafunzi aliyekuwa akiwahi kufika shuleni na kuchelewa kuondoka baada ya masomo.
Alisema baada ya kufanya ufatiliaji, ili kubaini aliwaza huenda mwanafunzi huyo alikuwa akiishi na mama wa kambo aliyekuwa mkali, jambo lililomfanya aone shuleni kuwa sehemu salama zaidi.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka walimu kuendelea kuwa karibu na wanafunzi wao na kuzingatia mazingira wanayotoka ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma na kijamii.
Aidha, aliwataka viongozi wa vijiji, kata, madiwani na jamii kwa ujumla kuwathamini walimu na kuwapa ushirikiano unaostahili.
Alisema jamii haipaswi kuwahukumu walimu wote kutokana na makosa ya mtu mmoja, bali inapaswa kutambua mchango wao na kuwaheshimu kwa kazi wanayoifanya.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Mragili, aliwapongeza walimu kwa kujituma na kufanya kazi kwa nidhamu, akisema juhudi zao zimechangia wilaya hiyo kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani.
Alisema Bukombe imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya Darasa la Nne, Darasa la Saba, Kidato cha Pili na Kidato cha Nne, huku katika matokeo ya Kidato cha Sita ikishika nafasi ya kwanza kimkoa.
Aliongeza kuwa wilaya hiyo imepiga hatua hadi kushika nafasi ya tisa kitaifa katika matokeo yaliyotajwa, jambo linaloonyesha kuwa walimu wamekuwa wakiongeza juhudi katika ufundishaji.
“Sisi Wilaya ya Bukombe hatushindani tena na mkoa pekee, bali viwango vimepanda na sasa tunaingia katika ushindani wa kitaifa katika ufaulu wa wanafunzi,” alisema Mhandisi Mragili.
Alisema mafanikio hayo yametokana na kujituma kwa walimu, huku serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Alifafanua kuwa Wilaya ya Bukombe inatarajia kujenga vyumba 313 vya madarasa, ambapo tayari ujenzi wa vyumba 10 umeanza.
Alisema hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya shule ili walimu na wanafunzi waweze kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, alisema katika kipindi cha miaka mitano watumishi wameajiriwa mkoani humo, wakiwamo walimu kati ya watumishi wapya.
Alisema walimu wa Bukombe wanaongoza kwa nidhamu kimkoa, huku serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maslahi ya watumishi.
Gombati alibainisha kuwa watumishi 17,338 wamepandishwa vyeo na 1,320 wamebadilishiwa kada mkoani Geita, wengi wao wakiwa walimu.Aliwataka walimu kuendelea kudumisha nidhamu, umoja na ushirikiano ili kuhakikisha sekta ya elimu inaendelea kupata matokeo mazuri.
Awali, akisoma risala kwa niaba ya kamati ya maandalizi, Jenipha Kisusi alisema maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani katika Wilaya ya Bukombe yalianzishwa mwaka 2018 na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Alisema tangu kuanzishwa kwake, maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka tarehe 8 au 9 Oktoba kwa lengo la kuwapongeza walimu na kutambua mchango wao katika maendeleo ya elimu.
Katika maadhimisho hayo, shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya mitihani na maeneo mengine ya kitaaluma zilitunukiwa vyeti na zawadi za fedha.
Kwa upande wa shule za msingi, Shule ya Msingi Kapwani ilipata Sh milioni moja, Lyobahika Sh 700,000 na Ilemela Sh 500,000.
Kwa shule za sekondari zilizofanya vizuri katika ufaulu, Shule ya Sekondari Bukombe ilipata Sh milioni moja, Butinzya Sh 700,000 na Busonge Sh 500,000.
Kwa upande wa shule za sekondari zinazotoa elimu ya Kidato cha Tano na Sita, Shule ya Sekondari Bukombe ilipata Sh milioni moja, Runzewe Sh 700,000 na Katente Sh 500,000.
Mbali na shule hizo, zawadi zilitolewa kwa walimu waliofanya vizuri katika ufundishaji wa masomo mbalimbali, wanafunzi waliofanya vizuri darasani, wakiwamo waliofanya vizuri katika uandishi wa insha, pamoja na walimu walioonyesha juhudi katika utunzaji wa mazingira.
Maadhimisho hayo yaliambatana na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, akiwamo Brother K na Juma Necha, na wasani wengine huku burudani nyingine zikitarajiwa kuendelea wakati wa sherehe za usiku.

Comments
Post a Comment