Na, Ernest Magashi
emagashi@bukombesasablog.com.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chipukizi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, Amos Festo, amewataka wazazi na walezi kuwaandaa watoto wao wanaoshiriki katika Jumuiya ya Chipukizi ili washiriki kikamilifu katika vikao na shughuli za jumuiya hiyo.
Festo alitoa wito huo wakati akisalimia wanachama wa CCM Kata ya Bukombe katika ziara ya Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, akiwa ameambatana na Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM wilayani humo.
Alisema ameambatana na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe katika ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake, huku akieleza kuwa anatarajia kuanza ziara katika kata zote 17 za Wilaya ya Bukombe kwa lengo la kukutana na Chipukizi na kuzungumza nao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu jumuiya hiyo.
“Nimeambatana na Mwenyekiti wa UVCCM katika utekelezaji wa majukumu yangu. Naomba wazazi na walezi, kuanzia ngazi ya matawi na mashina, kuwaandaa watoto wanaoshiriki katika Jumuiya ya Chipukizi. Hivi karibuni natarajia kufanya ziara katika kata zote 17 ili kukutana na Chipukizi na kuzungumza nao kuhusu masuala yetu,” alisema Festo.
Mwenyekiti huyo wa Chipukizi alisema ziara hiyo inatarajiwa kuanza mapema Novemba 2026, ambapo atatembelea kila kata, hivyo kuwaomba viongozi na wazazi kuwaandaa Chipukizi ili wawe tayari kumpokea na kushiriki katika shughuli hizo.
Aidha, aliwataka wazazi na walezi kutambua kuwa wana jukumu la msingi katika kuwalea watoto wao kuwa na maadili mema, kuwahimiza kusoma na kuhakikisha wanahudhuria vikao na shughuli za Jumuiya ya Chipukizi.
Kwa upande wake, Katibu wa Hamasa na Chipukizi Wilaya ya Bukombe, Mery Kapango, aliwataka viongozi na wajumbe wa Jumuiya ya Chipukizi kujiandaa kumpokea mwenyekiti wao wakati wa ziara hiyo na kuhakikisha wanatekeleza majukumu mengine yanayohusu jumuiya.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, aliwataka viongozi jumuia zote ndani ya CCM kuanzia ngazi ya matawi hadi kata kuhakikisha wanafanya vikao na kuendelea kuwaandaa vijana kushiriki katika shughuli za chama ili kufikia malengo yaliyowekwa na CCM.
Ndugu pia aliwahimiza vijana kuendelea kuunda vikundi na kuhakikisha vinasajiliwa kwa mujibu wa sheria ili viweze kuwanufaisha na fursa mbalimbali, ikiwemo mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.

Comments
Post a Comment