MWANAFUNZI MBARONI KWA TUHUMA ZA KUMUUA MWENZAKE

 
Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanafunzi Lameck Isack kwa tuhuma za kumuua mwanafunzi mwenzake, David Lucas, kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha kali katika sehemu za shingo na ubavu wa kulia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Oktoba 29, 2026, katika Kijiji cha Mhama, Kata ya Namonge, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.

Kamanda Jongo alisema kuwa kabla ya tukio hilo, vijana hao, ambao walimaliza kidato cha nne mwaka huu katika Shule ya Sekondari Said Nkumba, walikutana kwa mazungumzo wakiwa pamoja na wanafunzi wengine watatu.

Alisema kuwa wakiwa katika mazungumzo hayo, mabishano yalizuka baada ya kila mmoja kudai kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana mmoja. 

Hali hiyo ilisababisha ugomvi kati yao, ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumchoma David kwa kitu chenye ncha kali katika sehemu za shingo na ubavu wa kulia.Kutokana na majeraha hayo, David alifariki dunia muda mfupi baadaye.

Kamanda Jongo alisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini mazingira yote yaliyosababisha mauaji hayo, kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.

Aliongeza kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Aidha, Kamanda Jongo aliwataka wazazi na walezi kuimarisha malezi, maadili na ufuatiliaji wa mienendo ya watoto wao ili kuwajenga katika misingi ya uvumilivu, kuheshimiana na kutatua tofauti zao kwa njia za amani.

Comments