BUKOMBE
Shule ya Sekondari Ikuzi iliyopo Kata ya Runzewe Mashariki, Wilaya ya Bukombe, imefanya mahafali yake ya kwanza ya Kidato cha Nne tangu kuanzishwa mwaka 2023.
Mahafali hayo yameambatana na pongezi kwa Mbunge wa Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango wake katika kuboresha mazingira ya shule, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa maji, umeme, samani na mfumo wa kinga dhidi ya radi.
Mkuu wa shule, Abdulmajid Yusuph, amesema mafanikio yaliyofikiwa yametokana na ushirikiano wa Serikali, wazazi, walimu, viongozi na wadau mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Mussa Peter, amesema Ikuzi imepiga hatua katika taaluma na miundombinu, huku akieleza kuwa shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza kiwilaya kwa shule za Serikali katika matokeo ya Kidato cha Pili mwaka 2025.
Hata hivyo, shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa maabara, maktaba, jengo la utawala, nyumba za walimu, vifaa vya TEHAMA na tenki la maji.
Katika kuchangia utatuzi wa changamoto hizo, UVCCM Mkoa wa Geita imekabidhi kompyuta tatu zenye thamani ya Sh milioni 1.5, pamoja na fedha kwa ajili ya ukarabati wa choo cha walimu na mradi wa sabuni wa wanafunzi.
Shule ya Sekondari Ikuzi, ambayo kwa sasa ina walimu 16, imekuwa muhimu katika kutoa elimu kwa jamii za Ikuzi, Mlumbaga na Mpangwe.


Comments
Post a Comment