MAIGA FOUNDATION-TANZANIA YATOA MSAADA WA VIFAA KWA WANAFUNZI

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Jitegeme, iliyopo Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameishukuru Shirika la Maiga Foundation-Tanzania kwa kuwapatia msaada wa vifaa vya shule wanafunzi wenye uhitaji.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenye uhitaji shuleni hapo, Rehema Yohana, alilishukuru shirika hilo kwa kuwakumbuka na kuwajali wanafunzi wenye mahitaji mbalimbali.Naye mwanafunzi wa shule hiyo, Amos Iddy, alisema vifaa hivyo vitawasaidia katika masomo yao, hasa kwa kuwa baadhi yao walikuwa na uhitaji wa madaftari na vifaa vingine vya shule.

Alisema msaada huo pia umewapunguzia mzigo walezi wao ambao walikuwa wakihangaika kununua vifaa vya shule kwa ajili ya watoto wao.Kwa upande wake, Mwalimu wa Kitengo cha Hedhi Salama katika Shule ya Msingi Jitegeme, Lucy Komba, alisema kitendo kilichofanywa na Maiga Foundation-Tanzania ni cha kupongezwa, kwa kuwa kimewafurahisha wanafunzi na kuwasaidia kukabiliana na changamoto za mahitaji ya shule.

“Nawashukuru Shirika la Maiga Foundation-Tanzania kwa msaada walioutoa leo shuleni kwetu. Ni jambo jema na zuri, kwani tunahitaji msaada wa aina hii. Hapa kuna wanafunzi wengi wenye uhitaji, hivyo tunaomba wadau wengine wenye moyo wa kujitolea waendelee kuja na kusaidia mahitaji mbalimbali ya wanafunzi,” alisema Komba.Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Maiga Foundation-Tanzania Wilaya ya Bukombe, Frank Kaare, alisema shirika hilo limekabidhi madaftari 80 na boksi mbili za kalamu kwa wanafunzi wenye uhitaji.

Kaare aliwaomba wadau wengine kujitokeza na kuendelea kuwasaidia watoto pamoja na watu wenye mahitaji katika jamii.

Alisema Maiga Foundation-Tanzania itaendelea kugusa maisha ya jamii mbalimbali kwa kutoa misaada kulingana na uwezo wa shirika hilo.

Comments