Na, Ernest Magashi
emagashi@bukombesasablog.com.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, imeanza rasmi ujenzi wa nyumba nne za watumishi wa chama katika ngazi ya Wilaya.
Mradi huo wa ujenzi wa nyumba zinajengwa Kitongoji cha Buntubili, Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe, na hadi kukamilika zinatarajiwa kugharimu Shilingi 818,184,200.00, kwa mujibu wa BOQ ya ujenzi.
Nyumba hizo zinatarajiwa kutumika kama makazi ya Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe pamoja na makatibu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Jumuiya ya Wazazi.
Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya katika eneo la mradi na Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe, Leonard Mwakalukwa, amesema ujenzi wa nyumba hizo umefadhiliwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na wanachama wa CCM, akiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Mwakalukwa amesema ujenzi wa nyumba hizo ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya kazi na makazi kwa watumishi wa chama, pamoja na kuimarisha utekelezaji wa shughuli za chama katika Wilaya ya Bukombe.
Kwa upande wake, Dkt. Doto Biteko ameipongeza Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Bukombe kwa kuanza na kufikia hatua hiyo ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa chama, akisema hatua hiyo ni sehemu ya kujali na kuboresha ustawi wa watumishi hao.
Amesema ujenzi wa nyumba hizo utasaidia kuwawezesha watumishi wa chama kupata mazingira bora ya makazi na hivyo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wa chama na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kiutendaji katika mazingira bora.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe Matondo Lutonja amewataka wasimamizi wa mradi kuhakikisha ujenzi wa nyumba hizo unazingatia viwango vinavyotakiwa, ili ziwe imara, salama na ziweze kutumika kwa muda mrefu kwa lengo lililokusudiwa.

Comments
Post a Comment