DKT. BITEKO AKUTANA NA KAMATI YA MAANDALIZI YA SIKU YA MWALIMU DUNIANI BUKOMBE

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, amekutana na Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani, yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 9, 2026 katika ngazi ya Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.Maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ushirombo, ambapo Dkt. Biteko ameitaka kamati kuhakikisha siku hiyo inakuwa ya furaha, burudani na kumbukumbu nzuri kwa walimu wanaotarajiwa kushiriki.

Mratibu wa maadhimisho hayo, Mwalimu Abdulmajid Yusuph, amesema maandalizi yanaendelea vizuri, huku kamati ikiwa imejipanga kuhakikisha walimu wanapata fursa ya kufurahia siku yao.Amesema maandalizi yanazingatia upatikanaji wa chakula, vinywaji na burudani za kutosha, pamoja na shughuli mbalimbali zitakazowakutanisha walimu katika kusherehekea siku yao.

Kwa mujibu wa ratiba, shughuli zitaanza asubuhi kwa mashindano ya kwaya kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Bukombe, ambapo mshindi atapata nafasi ya kutumbuiza mbele ya mgeni rasmi.

Aidha, kutakuwa na michezo mbalimbali ikiwemo basketball, netball shootout na mchezo wa soka kati ya walimu wa Chuo cha Ualimu Katoke na timu ya Walimu wa Wilaya ya Bukombe.

Mbali na michezo, walimu watashiriki matembezi ya kuadhimisha siku hiyo, yatakayoanzia eneo la benki mjini Ushirombo na kuongozwa na brass band hadi katika uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo.

Shughuli hizo zitahitimishwa kwa Usiku wa Mwalimu, utakaokuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, akiwemo Juma Nature, Nandy, Chege, 20 Percent na Brother K.

Usiku huo pia utakuwa na mashindano ya rap freestyle, dancing competition pamoja na burudani nyingine zitakazolenga kuwapa walimu nafasi ya kujiburudisha na kusherehekea siku yao.Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Mwalimu Ramdhan Ng'oi, amesema kaulimbiu ya kamati hiyo ni “Wajibika Kumfanya Mwalimu Afurahi,” huku akiwataka wajumbe wote kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kufanikisha maadhimisho hayo.

Akizungumza na kamati hiyo, Dkt. Biteko amesema walimu ni miongoni mwa makundi makubwa ya watumishi wanaotekeleza majukumu muhimu katika jamii, akieleza kuwa mchango wao katika kujenga na kuendeleza taifa unapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa.Amesema baadhi ya nchi zilizoendelea zimewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu na kuwathamini walimu, akisisitiza kuwa kumjenga, kumthamini na kumpa mazingira bora mwalimu ni sehemu ya kujenga taifa lenye maendeleo.Dkt. Biteko ameitaka kamati kuhakikisha walimu wanapokelewa vizuri, ratiba inazingatiwa na kila shughuli iliyopangwa inatekelezwa kwa wakati, ili maadhimisho hayo yawe ya mafanikio na kuwaacha walimu na kumbukumbu nzuri.

Comments