DIWANI AKABIDHI UWANJA WA KUJENGA CHUMBA CHA MAZOEZI YA SHOTOKAN KARATE UYOVU

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

DIWANI wa Kata ya Uyovu, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Mathayo Kagoma, amewakabidhi vijana wanaoshiriki mchezo wa Shotokan Karate uwanja wenye ukubwa wa mita 50 kwa 100 kwa ajili ya kujenga chumba cha mazoezi pamoja na ofisi na miradi mbalimbali ya kuwawezesha kukuza vipaji na uchumi wao.

Kagoma akiwa na vijana eneo la uwanja amekabidhi uwanja huo ambao awali ulikuwa mali yake binafsi, baada ya kuvutiwa na juhudi za vijana hao katika mchezo wa Shotokan Karate na kuona umuhimu wa kuwashika mkono ili waweze kufanya mazoezi katika mazingira bora na salama.Alisema lengo ni kuwawezesha vijana kukuza mchezo huo kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa hadi Kanda ya Ziwa, huku wakitumia fursa hiyo kuendeleza vipaji na shughuli za kiuchumi.

Akikabidhi uwanja huo, Kagoma aliwaomba vijana kushirikiana katika ujenzi na kuahidi kuendelea kuwashika mkono katika hatua za mwanzo.Aidha, aliwataka vijana kuwa wabunifu katika kutafuta fursa za kiuchumi, ikiwemo kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili wanufaike na mikopo inayotolewa na Halmashauri pamoja na fursa nyingine za kiuchumi, ikiwemo kuanzisha kampuni.

“Vijana wa UVCCM, wanamichezo wa Shotokan Karate na mwanamasumbwi King Kiroboto, nimewapa uwanja huu wenye ukubwa wa hatua 50 kwa 100. Mshikamane, mjenge na muwe wabunifu, kwa sababu Wilaya ya Bukombe ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinapaswa kutumia ili kukuza uchumi wao na kuondokana na hali ya utegemezi,” alisema Kagoma.Kagoma pia aliwapongeza vijana hao kwa kujitokeza kufanya usafi wa mazingira katika Kata ya Uyovu Oktoba 3, 2026, akisema hatua hiyo imeamsha mwamko wa jamii katika kushiriki usafi wa mazingira.

Alisema baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa usafi ni barabara ya kuelekea Mwanza pamoja na barabara kuu ya lami inayounganisha Tanzania na nchi jirani, zikiwemo Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akizungumza baada ya kukabidhiwa uwanja huo, mwanamasumbwi wa kulipwa wa Wilaya ya Bukombe, Frank Paul, maarufu King Kiroboto, alisema wameupokea uwanja huo kwa furaha na watahakikisha unatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.King Kiroboto, ambaye hushiriki mashindano ya ngumi ndani na nje ya Tanzania, alimwomba Diwani Kagoma kuendelea kuwashika mkono vijana ili waweze kufikia malengo yao.

Alisema kukamilika kwa chumba cha mazoezi kutawapa vijana sehemu nzuri, tulivu na salama ya kufanya mazoezi na kuendeleza vipaji vyao.Naye mwanafunzi wa Shotokan Karate, Meshaki Kionzo, aliwashukuru viongozi wa mchezo huo kwa kujenga mahusiano mazuri na viongozi wa chama na serikali, jambo ambalo amesema limewezesha vijana kupata uwanja huo.

Alisema uwanja huo utajengwa chumba cha mazoezi pamoja na kuanzisha miradi mingine ya kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.Naye mwanafunzi wa Shotokan Karate Kata ya Uyovu, Oliva Stanilaus, alimshukuru Diwani Kagoma na kusema ana ndoto ya kuwa mwanamichezo wa ngumi za kulipwa.

Alisema uwanja huo ukijengwa na kuwa na chumba kizuri cha mazoezi, utampa nafasi nzuri ya kufanya mazoezi na hatimaye kufikia malengo yake ya kimichezo.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Shotokan Karate Wilaya ya Bukombe na Kanda ya Ziwa, Safari Boniphance, maarufu Sensei, alimshukuru Diwani Kagoma kwa kuwaona vijana na kuwapatia uwanja kwa ajili ya kujenga chumba cha mazoezi kitakachotumika katika ngazi ya Kanda ya Ziwa.Sensei alisema yuko tayari kujitoa kufundisha vijana na kuhakikisha wanapata mafunzo bora yatakayowawezesha kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.Mwenyekiti wa Shotokan Karate Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, alisema kitendo cha Diwani Kagoma kuwapatia vijana uwanja huo ni hatua inayotambua nafasi ya vijana na dhamira yao ya kujenga maisha yao kiakili na kiuchumi.

Ndugu alisema wameupokea uwanja huo na watautunza, huku wakiahidi kutekeleza ushauri walioupata kutoka kwa Diwani, ikiwemo kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayosaidia vijana kujipatia kipato baada ya ujenzi kukamilika.Aidha, aliwasisitiza vijana wa kiume na wa kike kuendelea kufanya mazoezi na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali.

Pia aliwahimiza kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba (Mgambo) yatakapotangazwa na serikali, akisema hatua hiyo inaweza kuwajengea sifa na nidhamu pamoja na kuwaongezea fursa katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa mujibu wa taratibu na sheria.

Comments