emagashi@bukombesasablog.com.
Walimu wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, wameagizwa kutumia mashamba ya shule kulima mazao ya lishe yatakayosaidia kuongeza upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, Ally Mketo, Oktoba 30, 2026, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Katome.
Mketo alisema jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula wanapokuwa shuleni linahitaji ushirikiano wa walimu, viongozi wa shule, wazazi na jamii kwa ujumla.
Aliwataka watendaji wa kata, walimu wakuu na wakuu wa shule kuhakikisha kila mwanafunzi anapata angalau mlo mmoja akiwa shuleni, akisisitiza kuwa lishe bora ni sehemu muhimu ya ustawi, afya na maendeleo ya mtoto.
Aidha, alihimiza kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe ili kuimarisha juhudi za kuhakikisha watoto wanapata chakula wanapokuwa shuleni.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Yohana Fumbuka, alisema lishe bora ni msingi wa afya na ukuaji wa watoto, huku ikichangia kuongeza uwezo wa wanafunzi kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za shule.
Naye Afisa Lishe wa Wilaya, Praygod Charles, aliwahimiza wananchi kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yao, ikiwemo nafaka na mizizi, vyakula vya jamii ya kunde, mbogamboga, matunda na vyakula vingine vya asili vinavyopatikana kulingana na misimu.
Maadhimisho hayo yalifanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Imarisha Afya, Kula Kiasili, Punguza Sukari, Chumvi na Mafuta,” inayohimiza jamii kuchagua vyakula vya asili, kuandaa mlo kamili kwa kuzingatia njia bora za mapishi na kupunguza ulaji wa sukari, chumvi na mafuta kwa wingi.
Ujumbe wa maadhimisho hayo umesisitiza umuhimu wa shule, wazazi na jamii kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata chakula chenye virutubisho muhimu kwa ajili ya afya bora, ukuaji na maendeleo yao kitaaluma.

Comments
Post a Comment