BUKOMBE KUSHUHUDIA BURUDANI KUBWA SIKU YA MWALIMU, DKT. BITEKO AWAKARIBISHA WANANCHI

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

MBUNGE wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, amewaalika walimu wa Wilaya ya Bukombe pamoja na wananchi kwa ujumla kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yatakayofanyika Oktoba 9, 2026, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ushirombo.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza saa 4:00 asubuhi, huku Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe.

Maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka wilayani Bukombe kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa walimu katika kutoa elimu na kujenga jamii yenye maarifa na ujuzi.Kupitia maadhimisho hayo, walimu watapata fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazolenga kutambua na kuenzi nafasi yao katika maendeleo ya elimu na jamii kwa ujumla.

Mbali na shughuli za mchana, maadhimisho hayo yataendelea usiku kwa burudani mbalimbali, ambapo wasanii maarufu wa muziki nchini wanatarajiwa kutumbuiza.

Miongoni mwa wasanii wanaotarajiwa kutumbuiza ni Juma Nature, Chege, Twenty Percent na Brother K, pamoja na wasanii wengine.Dkt. Biteko amewataka walimu na wananchi wa Bukombe kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho hayo na kupata burudani zitakazotolewa usiku.


Comments