BUKOMBE DC YATOKA SARE NA KATOKE TIC 1-1 KUELEKEA SIKU YA WALIMU

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

TIMU za soka za walimu wa Wilaya ya Bukombe (Bukombe DC) na Chuo cha Ualimu Katoke (Katoke TIC) zimetoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Bukombe Stadium, usiku wa kuamkia maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani yanayofanyika leo, Oktoba 9, 2026, wilayani Bukombe, mkoani Geita.Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulishuhudia Bukombe DC ikianza kwa kasi, ikifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya pili kupitia kwa mwalimu John Aule, aliyeitumia vyema nafasi hiyo kuipa timu yake matumaini ya kupata ushindi.Hata hivyo, Katoke TIC haikukubali kulala mbele, kwani dakika ya 29, mwalimu Yohana Elias aliisawazishia timu yake kwa kufunga bao lililorejesha matumaini na kuufanya mchezo huo kuwa na ushindani mkali zaidi.

Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, matokeo yaliyoendelea kudumu hadi dakika 90 za mchezo zilipokamilika.Katika kipindi cha pili, makocha wa timu zote mbili walifanya mabadiliko mbalimbali wakilenga kuongeza nguvu katika safu zao za ushambuliaji ili kupata bao la ushindi. Hata hivyo, safu za ulinzi za timu hizo zilisimama imara na kuzuia mabao zaidi, hivyo mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.Mchezo huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi pamoja na viongozi mbalimbali, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, na wageni waalikwa walioshiriki katika shughuli za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani wilayani humo.Mchezo huo ni sehemu ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Walimu Duniani, inayowakutanisha walimu na wadau mbalimbali katika kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano kupitia michezo.

Comments