Na, Ernest Magashi
ebukombesasablogspot.com.tz
Wananchi na vijana wa Kata ya Bugelenga, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango wake katika kuhamasisha na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.
Pongezi hizo zimetolewa baada ya Dkt. Biteko kuchangia mifuko 130 ya saruji kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Bugelenga.
Akizungumza mbele ya Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu aliyekuwa na ziara ya kwenda anaagalia uhai wachama na jumuia zake, Katibu wa CCM Kata ya Bugelenga, Ramadhan Mlagwa, alisema wananchi wanampongeza Dkt. Biteko kwa kuendelea kushirikiana nao katika kuchochea maendeleo.
Mlagwa alisema kati ya mifuko hiyo 130 ya saruji, mifuko 30 imetolewa kwa ajili ya ujenzi na upakaji wa lipu katika Ofisi ya CCM Kata ya Bugelenga, huku mifuko 100 ikitumika katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi moja ya utawala katika Shule ya Sekondari Bugelenga.
Kaka Mkuu wa Shule ya Sekondari Bugelenga, Elikana Samson Kisimba, alimshukuru Dkt. Biteko kwa kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu ya shule hiyo, akisema kukamilika kwa ujenzi huo kutawawezesha wanafunzi kupata mazingira bora zaidi ya kujifunzia.
Naye dada mkuu wa Shule hiyo, Ester Musa, alisema ni jambo la kufurahisha kuwa na kiongozi anayejali maendeleo ya wananchi, hasa katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa ajili ya wanafunzi na walimu.
Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Musa Mwabubili, alisema ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya utawala ulianza Agosti mwaka huu na unaendelea.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, aliwaomba wananchi na wanachama kuendelea kumuunga mkono Mbunge huyo katika juhudi zake za kusukuma maendeleo kwa kushirikiana na Serikali.
Ndugu alitembelea kuona ujenzi na barabara huku akisisitiza ushirikiano kati ya wananchi, viongozi na Serikali ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa na kuleta manufaa kwa jamii.

Comments
Post a Comment