WANACHAMA WA CCM WAMPONGEZA DKT. BITEKO KWA KUCHANGIA UJENZI WA OFISI YA CCM KATOME

Na, Ernest Magashi

emagashi@bukombesasablog.com.tz

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Katome, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuchangia ujenzi wa ofisi ya CCM ya kata hiyo, unaoendelea.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Katome, Erasto Maswangwa, wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, pamoja na Kamati ya Utekelezaji, iliyolenga kukagua uhai wa chama na jumuiya zake katika Kata ya Katome.Maswangwa alisema katika ujenzi wa ofisi hiyo, Dkt. Biteko amechangia mifuko 100 ya saruji, tofali 1,000 pamoja na Shilibgi milioni mbili, ikiwa ni sehemu ya kusaidia kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo baada ya wanachama kuchangia fedha na kununua eneo la ujenzi.Alisema mchango huo ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na Dkt. Biteko katika kuhamasisha maendeleo ndani ya chama na kwa wananchi wa Jimbo la Bukombe.Maswangwa alimuomba Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe kufikisha pongezi hizo kwa Dkt. Biteko, akisema wanachama wanatambua mchango wake katika kuimarisha chama na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, aliahidi kufikisha pongezi hizo kwa Dkt. Biteko, huku akisema mbunge huyo amekuwa akishirikiana na chama kuanzia ngazi ya matawi na mashina hadi wilaya.

Ndugu alisema ushirikiano huo umeendelea kuchangia katika kuimarisha chama na kuchochea shughuli za maendeleo kwa wananchi.Katika ziara hiyo, Ndugu aliwataka viongozi wa jumuiya ngazi ya matawi na mashina kuhakikisha wanachama wanasajiliwa kwa njia ya kielektroniki, pamoja na kuhamasisha wanachama na jumuiya zao kulipa ada za chama kwa wakati.

Pia aliwataka viongozi hao kufanya vikao mara kwa mara ili kubaini changamoto zinazowakabili wanachama na kutafuta njia za kuzitatua.Aidha, aliwahamasisha vijana kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yao, ikiwemo mikopo inayotolewa na Halmashauri, ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Katome, Eva Petro, alisema vijana wako tayari kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya kwa kufanya vikao na kuunda vikundi vya kiuchumi, ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali, ikiwemo mikopo inayotolewa na Halmashauri.

Comments