Na,Irene Makopudo,Geita
imakopudo@bukombesasablog.com.tz
Mkuu wa Wilaya ya Chato Louis Bura alipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa hatua ya kusambaza umeme katika maeneo 52 ya wachimbaji wadogo huku akisema huduma hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Bura alisema hayo alipotembelea Banda la Tanesco kwenye maonyesho ya madini yanayoendelea mkoani Geita ambapo amesema kuwa huduma za umeme katika Mkoa wa Geita huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na TANESCO kwa kutoa taarifa kuhusu changamoti za huduma hiyo ili ziweze kutatuliwa kwa wakati.
Alisema matumizi ya mifumo ya mawasiliano ya kidijitali ikiwemo makundi ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali, yamesaidia kurahisisha utoaji wa taarifa za changamoto za umeme na kupunguza malalamiko ya wananchi.
“Ushirikishwaji wa wananchi katika kutoa taarifa kuhusu changamoto za huduma ya umeme ni muhimu kwa sababu unasaidia changamoto hizo kufanyiwa kazi kwa wakati.
Vilevile Bura alisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia nishati safi, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira.Serikali imeendelea kuweka msisitizo katika matumizi ya nishati safi na kwamba TANESCO ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika kuhamasisha utekelezaji wa ajenda hiyo.
"Ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira ni changamoto kubwa. Juhudi zinapaswa kuongezwa kuhakikisha tunaendelea kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ili kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo,” alisema Bura.
Alilitaka Shirika la TANESCO kuendelea kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi pamoja na maeneo yenye shughuli za uzalishaji, akisema upatikanaji wa umeme ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Mkoa wa Geita, Lucas Swere alisema TANESCO imekamilisha kusambaza umeme katika karibu vijiji na maeneo 52 ya wachimbaji wadogo, hatua ambayo imewawezesha wananchi kutumia nishati hiyo katika shughuli za uchimbaji na shughuli nyingine za kiuchumi.
"Tumekamilisha kupeleka umeme katika karibu vijiji na maeneo 52 ya wachimbaji wadogo. Sehemu kubwa ya wananchi sasa wanatumia umeme katika shughuli zao za uchimbaji alisema Swere.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za TANESCO kuhakikisha maeneo yenye shughuli za uzalishaji yanafikiwa na huduma ya umeme hivyo kuwawezesha wananchi kuongeza ufanisi katika shughuli zao.
Mbali na kusambaza umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo, Swere alisema TANESCO imejipanga kushiriki katika utekelezaji wa ajenda ya Serikali ya matumizi ya nishati safi na utunzaji wa mazingira.
Aidha wananchi wanaendelea kuhamasishwa kuachana na matumizi ya nishati zinazochafua mazingira na kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi, ikiwemo matumizi ya majiko yenye teknolojia za kisasa.Katika maonyesho hayo, TANESCO imeonyesha aina mbalimbali za majiko yanayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika kaya.
"Lengo letu ni kuhamasisha wananchi wote kutumia nishati safi badala ya nishati chafu. Tunawaalika wananchi kufika katika banda la TANESCO kujifunza namna wanavyoweza kusaidia kulinda mazingira na kurahisisha shughuli za upishi katika nyumba zao", alisema Swere.
Comments
Post a Comment