Na, Ernest Magashi
emagashi@bukombesasablog.com.
Mtu mwenye ulemavu wa viungo, mkazi wa Mtaa wa Kapela, Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Sara Wiliam (53), amewaomba Watanzania kumsaidia kupata baiskeli maalumu ya watu wenye ulemavu pamoja na mtaji ili aweze kujikwamua kiuchumi.
Sara ametoa ombi hilo baada ya kukabidhiwa msaada wa sukari, sabuni ya mche na mahitaji mengine ya nyumbani na Mwenyekiti wa Shirika la Maiga Foundation-Tanzania, Frank Kaare.
Akizungumza, Sara alisema alizaliwa akiwa mzima, lakini alipata ulemavu wa viungo akiwa na umri wa miaka mitano baada ya kuugua.
Alisema changamoto kubwa anayokabiliana nayo ni usafiri, hali inayomfanya ashindwe kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kwenda kanisani, sokoni na kuhudhuria misiba ya ndugu, jamaa na majirani.
“Naomba Watanzania wenzangu wanisaidie kupata baiskeli ya watu wenye ulemavu ambayo itanisaidia kwenda kanisani kusali, sokoni na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo misiba. Kwa sasa mara nyingi nashindwa kwenda kwa sababu sina usafiri,” alisema Sara.
Sara pia aliomba kusaidiwa mtaji ili aweze kuongeza shughuli zake za kujipatia kipato na kuboresha maisha yake pamoja na familia inayomtegemea.
Alisema amekuwa akijishughulisha na kupasua na kuuza kokoto, huku awali akiwa amewahi kuuza mgahawa, kufinyanga vyungu na kuuza mkaa.
Hata hivyo, alisema biashara ya kokoto inakabiliwa na changamoto ya kutopata wateja kila siku, huku akieleza kuwa anaweza kupasua ndoo moja na kuiuza kwa Sh300, na kutokana na hali yake hawezi kuzalisha zaidi ya ndoo tano kwa siku.
Sara alisema anaishi katika mazingira magumu na wakati mwingine hutegemea msaada wa wasamaria wema ili kupata mahitaji ya kila siku.
“Katika kujikimu kwa kila siku kuna wasamaria wema ambao hunisaidia kwa chochote. Mtu akipita ananipa hata kiasi kidogo, ninanunua chakula tunakula. Nikifanya kazi ya kuuza kokoto tunapata chakula. Kwa kifupi, naishi katika mazingira magumu, ndiyo maana naomba msaada kwa Watanzania wenzangu,” alisema.
Mbali na msaada wa baiskeli na mtaji, Sara aliomba pia Watanzania wenye uwezo kumsaidia kupata makazi bora kutokana na mazingira magumu anayoishi pamoja na majukumu ya familia nyumba anayoishi wakati wa masika inavuja.
Alisema hana mme ila naishi na wajukuu watano, ambapo mmoja ni mtoto wa marehemu mwanawe na wengine ni wajukuu wa ndugu zake ambao tayari wametangulia mbele za haki.
Mwenyekiti wa Shirika la Maiga Foundation-Tanzania, Wilaya ya Bukombe Frank Kaare, alisema shirika hilo limekuwa likimtembelea Sara mara kwa mara na kumsaidia mahitaji mbalimbali kulingana na uwezo wao.
Kaare aliwaomba wadau wa maendeleo, mashirika na watu binafsi wenye uwezo kujitokeza kumsaidia Sara kupata baiskeli maalumu pamoja na mtaji ili aweze kuendelea na shughuli za kujipatia kipato na kushiriki katika shughuli za kijamii.
“Tunawaomba wadau wa maendeleo na mashirika mengine kuona umuhimu wa kumsaidia mama huyu. Ana kiu ya kupata baiskeli itakayomrahisishia kufika kanisani na kujumuika na jamii katika shughuli mbalimbali,” alisema Kaare.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kapela, Harold Sambali, alisema Sara ni mkazi wa mtaa huo na anaifahamu changamoto anayopitia kutokana na ulemavu wake.
Sambali alisema amewahi kumtembelea Sara na kuona mazingira anayoishi, akibainisha kuwa anahitaji msaada, hasa wa kupata baiskeli itakayomrahisishia kutembea na kushiriki katika shughuli mbalimbali.
Alisema licha ya yeye kufahamu changamoto hizo, Diwani wa eneo hilo pia anazifahamu hali na mahitaji ya Sara.
Mwenyekiti huyo aliomba mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi na wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia Sara ili kupunguza changamoto anazokabiliana nazo katika maisha ya kila siku pamoja na familia inayomtegemea.

Comments
Post a Comment