Na, Ernest Magashi
Mwanamichezo wa ngumi za kulipwa, Frank Paul maarufu King Kiroboto, ameomba kuandaliwa kwa pambano la Kickboxer wilayani Bukombe mkoani Geita, litakalowakutanisha wapiganaji kutoka nje ya wilaya na mkoa huo.
King Kiroboto amesema yuko tayari kupanda ulingoni na kupambana na wapiganaji mbalimbali, akieleza kuwa anaamini pambano hilo likifanyika Bukombe litakuwa fursa ya kuibua vipaji vya vijana na kuitangaza wilaya hiyo kupitia michezo ya kickboxer.
Ombi hilo lilitolewa wakati Afisa Michezo wa Wilaya ya Bukombe, Jenipha Kisus, alipokuwa akitoa elimu kwa vijana wanaojihusisha na michezo ya Shotokan Karate na ngumi za kulipwa kuhusu umuhimu wa kujisajiri Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ili umoja wao utambulike kisheria.
Akitoa elimu hiyo, Kisus aliwapongeza vijana hao kwa kuwa na umoja, kufanya mazoezi na kuendelea kutafuta fursa kupitia michezo, akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuitangaza Bukombe katika sekta ya michezo.
Aliwataka vijana hao kuhakikisha wanajisajili BMT kwa kufuata taratibu zinazotakiwa, ikiwemo kujaza taarifa muhimu na kulipa ada za usajili.
Kisus alisema baada ya vijana hao kukamilisha usajili, kutakuwa na uwezekano wa kuandaa mashindano mbalimbali ya michezo, ikiwemo pambano la Kickboxer, jambo ambalo linaweza kuwapa wananchi burudani na pia kuwasaidia vijana kutumia vipaji vyao kama ajira na chanzo cha kipato.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Ngumi na Shotokan Karate Wilaya ya Bukombe, Safari Bonifas maarufu Seisei, alimshukuru Afisa Michezo kwa elimu hiyo, akisema imewapa uelewa zaidi kuhusu umuhimu wa kuwa na umoja na kufuata taratibu za kisheria.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Shotokan Karate Wilaya ya Bukombe na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukombe, Nelvin Ndugu, alimshukuru Afisa Michezo kwa kutoa elimu hiyo kwa vijana.
Ndugu alisema lengo la vijana hao ni kuona vipaji vyao vinaendelea na kupata fursa za kushiriki mashindano ya kulipwa ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Aliwataka vijana kuendelea kushikamana, kuzingatia elimu waliyopewa na Afisa Michezo na kushirikiana na wadau wa michezo ili kuhakikisha mashindano ya ngumi yanafanyika wilayani Bukombe.
Akizungumzia safari yake katika ngumi za kulipwa, King Kiroboto alisema jina lake kamili ni Frank Paul, akiwa mkazi wa Kata ya Uyovu wilayani Bukombe, na alianza safari ya kutafuta nafasi katika ngumi za kulipwa mwaka 2020.
Alisema safari yake ilimpeleka Dar es Salaam, ambako alianza kutafuta nafasi ya kushiriki mapambano ya Kickboxer.
Kwa mujibu wa King Kiroboto, mwaka 2023 alipata nafasi ya kwanza ya kupanda ulingoni kama mchezaji wa kulipwa katika mashindano yaliyofahamika kama Wababe wa Kitaa (WWK) yaliyofanyika Dar es Salaam.
Alisema katika mashindano hayo alipigana mapambano matano, akashinda matatu, akapoteza moja na kuendelea hadi hatua ya nusu fainali.
King Kiroboto alisema mwaka 2024 alipata pambano lingine la Professional Kickboxer Dar es Salaam na kufanikiwa kushinda, kabla ya kupata nafasi ya kushiriki pambano la Professional Boxer mjini Dodoma, ambako pia alifanikiwa kupata ushindi.
Aidha, alisema Juni 6, 2026 alipata nafasi ya kushiriki pambano la kulipwa nchini Rwanda, lililowakutanisha wapiganaji kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambapo alifanikiwa kumaliza akiwa mshindi wa pili.
Akielezea mpambano anaoutamani iwapo pambano la Kickboxer litaandaliwa Bukombe, King Kiroboto alisema anatamani kukutana tena na bondia Said Nyamaume, ambaye anamuelezea kuwa ni mmoja wa mabondia anaotamani kupambana naye.
“Kama pambano likiitishwa Bukombe, natamani sana kurudiana na Said Nyamaume. Ningefurahi sana kama angekuja nyumbani Bukombe na tukapanda naye ulingoni,” alisema King Kiroboto.
Aidha, alisema katika upande wa Boxer anatamani pia kupata nafasi ya kupambana na Said Bwanga, akisisitiza kuwa yuko tayari kupanda ulingoni wakati wowote nafasi hiyo itakapopatikana.
King Kiroboto amesema yuko tayari kuendelea kufanya mazoezi na kutafuta mapambano yatakayomsaidia kukuza kipaji chake pamoja na kuitangaza Bukombe kupitia ngumi za kulipwa.


Comments
Post a Comment