Na, Ernest Magashi
Timu 17 zimefanikiwa kufuzu kutoka ngazi ya kata na kutinga hatua ya Tarafa katika mashindano ya KNK Cup 2026, baada ya kutwaa ubingwa katika kata zote 17 za Wilaya ya Bukombe.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati ya Mashindano ya KNK Cup 2026 Wilaya ya Bukombe, Domician Kabalenga, alipokuwa akizungumza na Bukombe Sasa Media kuhusu maendeleo ya mashindano hayo yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Kabalenga alisema mashindano hayo yalianza Julai 1, 2026 katika viwanja vya kata zote 17 za Wilaya ya Bukombe, yakishirikisha jumla ya timu 248 zilizoshindana kwa mfumo wa mtoano hadi Agosti 3, 2026.Kufikia hatua hiyo, timu 231 zilikuwa zimeondolewa huku timu 17 zikifanikiwa kutwaa ubingwa wa kata na kufuzu hatua ya Tarafa.
Alisema Ligi ya KNK Cup 2026 ngazi ya Tarafa itaanza rasmi Agosti 10, 2026, ambapo timu hizo 17 zitachuana kutafuta mabingwa wa Tarafa. Alifafanua kuwa Tarafa tatu zitakuwa na timu nne kila moja, huku Tarafa moja ikiwa na timu tano kutokana na mgawanyo wa kata.
"Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kushuhudia michezo ya ngazi ya Tarafa kama walivyofanya katika hatua ya kata. Ushabiki wao utawapa morali wachezaji na kuongeza hamasa ya mashindano," alisema Kabalenga.
Alieleza kuwa timu zitashindana katika Tarafa za Bukombe, Ushirombo, Siloka, Ng'anzo na Bulega kwa mfumo wa mtoano. Timu zitakazoshinda zitafuzu hatua zinazofuata hadi kupatikana mabingwa wa Tarafa watakaoendelea na hatua nyingine za mashindano.
Kabalenga pia aliwahamasisha wananchi kutumia fursa ya mashindano hayo kufanya biashara mbalimbali katika viwanja vya michezo ili kuongeza kipato chao.
Aidha, alisema KNK Cup 2026 imeendelea kuwa chachu ya kuibua vipaji vya vijana wengi, huku baadhi ya wachezaji wakipata nafasi ya kuonekana na kusajiliwa na timu zinazoshiriki ligi za madaraja ya juu nchini kupitia mashindano hayo.

Comments
Post a Comment