- Get link
- X
- Other Apps
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko alisema kuwa angependa kuona wananchi wa Kahama wanashirikiana na kuungana kwa pamoja katika shughuli za maendeleo ya Wilaya yao.
Amewaasa kutoacha msingi wa Chama Cha Mapinduzi wa kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba Taifa linategemea CCM iwahudumie na sio kuruhusu mipasuko miongoni mwao.
Dkt. Biteko aliyasema hayo Kahama, mkoani Shinyanga wakati aliposhiriki Mkutano Maalum wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Msalala uliolenga kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025.
Akizungumzia fursa za maendeleo zilizopo wilayani humo, Dkt. Biteko alisema kuwa Kahama ni Wilaya ya kimkakati ambayo ina bandari kavu iliyopo Isaka pia kitajengwa kiwanda cha kuchenjua madini pamoja na uwepo wa barabara inayoounganisha nchi za maziwa makuu.
“ Kutokana na uwepo wa fursa hizi tukishindwa kuungana tukashughulika na maendeeo ya watu basi watatushangaa. Nataka nitoe wito, pendaneni, shikamaneni Mungu amewapa kila aina ya utajiri tumieni fursa hiyo kujiletea maendeleo kwenye wilaya yenu na msiruhusu mipasuko katika chama chetu,” alisema Dkt. Biteko.
“Nawaomba baada ya mkutano huu tutoke hapa tukiwa wamoja na tuweke mbele maslahi ya Chama chetu na watu wetu,”aliongeza DKT. Biteko.
Dkt. Biteko amempongeza Mbunge wa Jimbo la Msalala, kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha wananchi wa Jimbo hilo wanapata miradi ya maendeleo na hivyo kutatua changamoto walizokuwa nazo hapo awali.
Awali Dkt. Biteko alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi katika Jimbo hilo ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali kwenye maji, elimu, afya na Barabara.
“ Mhe. Rais Samia amefanya makubwa katika nchi yetu, leo tunazungumza kuhusu miradi mingi na mikubwa hapa Kahama, tunazungumzia kujengwa kwa barabara ya Kakola kwa kiwango cha lami. Amefanya uchimbaji madini ubaki kwenye maendeleo yetu anataka uwepo wa miradi mingi zaidi ya barabara na maji niwaombe tumuombee ili aendelee kutimiza haya kwa ajili ya Watanzania,” alisema Dkt. Biteko.
Aliongeza kuwa Mhe. Rais Samia bado ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata maendeleo na kuishi katika mazingira bora zaidi.
“ Wito wangu kwenu shikamaneni, pendaneni, vumilianeni tukijenge Chama chetu ikiwa muda utafika wakati wa uchaguzi basi chagueni anayefanya kazi mwacheni anayesema watu. Mhe. Mbunge Iddi endelea kuchapakazi kwa maendeleo ya Jimbo lako,” Alisisitiza Dkt. Biteko.
Mbunge wa Jimbo la Msalala lililopo Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Iddi Kassim Iddi wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Jimbo hilo kwa Mwaka 2020 hadi 2025 amempongeza Dkt. Biteko kwa hatua ya kuendeleza sekta ya nishati kwa kusaidia vitongoji vyote vya Jimbo hilo kupata umeme.
Serikali inaendelea na azima yake ya kusambaza huduma za umeme katika vijiji vyote nchini. Hapa tumejulishwa kuwa Msalala ina jumla ya vijiji 92, ambavyo vyote vimefikiwa na huduma ya umeme, kazi iliyobaki ni kupeleka umeme kwenye vitongoji.
Akizungumzia sekta ya maji Iddi alisema mwaka 2020 hadi 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mfano ametoa sh 2 bilioni kwa ajili ya miradi ya kusambaza maji katika vijiji mbalimbali Jimbo la Msalala.
Iddi alisema mafanikio ya miradi hiyo imesaidia Jimbo hilo ambalo kwa sasa wanaendelea kusambaza maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo hususani katika vitongoji na tayari Serikali imeshaleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“ Wakati naingia madarakani miradi ya maji ilikuwa kwa asilimia 25 pekee na sasa miradi ya maji imefikia asilima 95,” alisema Mhe. Iddi.
Kwa upande wa sekta ya elimu alisema Rais Samia ameboresha sekta hiyo kwa kutoa fedha zilizosaidia katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa, mabweni na maabara.
“ Tumekuwa na shule nyingi maana yake tutawasomesha watoto wetu kwa kiwango cha kutosha, pia tumeanzisha ujenzi wa Chuo cha VETA na kitakapo kamilika kitakuwa na manufaa makubwa kwa jamii hususan vijana ili wapate ujuzi na kuajirika katika soko la ajira,” alisema Mhe. Iddi.
Mhe, Iddi akizungumza barabara alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano Jimbo hilo kwa kushirikiana na TARURA wamefungua barabara nyingi ikiwemo barabara inayotoka Kakola kwenda Kahama ambayo kwa sasa inapitika vizuri.
Mhe, Iddi alimshukuru Rais Samia kwa kutekeleza Ilani ya CCM katika Jimbo hilo kwa asilimia 99.9.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment