Msemaji mkuu, wa Serikali ambaye pia ni katibu mkuu wa Wizara ya Habari Sanaa na Michezo Gerson Msigwa kifafanua jambo katika ufunguzi wa Warsha maalum kwa Wahariri na Waandishi wa habari kuelekea mkutano mkuu wa nishati wa wakuu wa nchi za afrika uliofanyika Leo January 5. 2025 jijini Dar es salaam
Dar es salaam - Msemaji mkuu, wa Serikali ambaye pia ni katibu mkuu wa Wizara ya Habari Sanaa na Michezo Gerson Msigwa, amesema Tanzanian imezidi kuwa kinara kwenye Sekta ya Nishati barani Afrika.
Akizungumza wakati akifungua Warsha maalum ya Wahariri na Waandishi wa habari Nchini uliofanyika Leo January 5. 2025 jijini Dar es salaam
Amesema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa unaolenga kuharakisha ukuaji wa mageuzi katika nishati barani Afrika.
"Tukio hili linatufanya kuwa kitovu cha mjadala wa kimataifa kuhusu nishati ya umeme endelevu".
Kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa kama Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na Umoja wa Afrika, tunalenga kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme bora, nafuu, na endelevu kufikia waafrika milioni 300 kufikia mwaka 2030.
Aidha Msigwa amesema Kupitia nafasi hii, Tanzania inaonyesha dhamira yake ya kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya nishati ya umeme barani Afrika, ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa umeme vijijini na mijini.
"Umeme ni uti wa mgongo wa maendeleo yetu ya kiuchumi na kijamii. Kupitia miradi mikubwa kama Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Tanzania imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa umeme ambao mpaka sasa tunazalisha megawati 1,410 kutoka katika mashine sita na tunatarajia mwaka huu mradi kukamilika".
Mwaka 2020 hadi 2024, Serikali imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 12,278, sawa na asilimia 99.7 ya vijiji vyote.
Aidha, Vitongoji 32,827 vimefikiwa na umeme kati ya vitongoji 64,359 sawa na asilimia 51 ikiongeza uwezekano wa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Hatua hizi zimeimarisha sekta za elimu, afya, biashara, na usafiri, ambapo taasisi za afya na elimu zaidi ya 12,905 zimeunganishwa na umeme, na kusaidia kuinua viwango vya utoaji huduma kwa wananchi"
Amesema kuwa uwekezaji katika vyanzo mbadala vya nishati kama vile umeme jua, jotoardhi, na upepo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme kwa megawati 1,100. Juhudi hizi zinalenga kuvutia uwekezaji katika Sekta ya viwanda, ambapo idadi ya viwanda vya uzalishaji wa vifaa vya nishati kama nguzo na nyaya imeongezeka kutoka 23 mwaka 2020 hadi kufikia viwanda 78 mwaka 2024.
Uzalishaji wa ndani wa vifaa hivi si tu unatoa ajira kwa Watanzania bali pia unapunguza gharama za miradi ya usambazaji nishati vijijini na mijini
Katika hatua nyingine Msigwa amesema Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kinara wa nishati safi ya kupikia Barani Afrika, huku akiweka ajenda ya nishati safi ya kupikia kama mojawapo wa kipaumbele cha kitaifa.
Kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia wa mwaka 2024 - 2034 Mkakati ambao aliuzindua mwaka 2024, tumedhamiria kufikia asilimia 80 ya kaya kuwa na nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
"Hatua hii ni muhimu si tu kwa kuboresha afya za wananchi wetu bali pia kwa kulinda mazingira yetu dhidi ya uharibifu wa misitu unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa". Amesema Msigwa".
Comments
Post a Comment