UTAFITI WA JIOLOJIA YA MIAMBA NA UDONGO KWA KURUSHA NDEGE NYUKI (DRONE) WAHAMIA SHINYANGA NA GEITA




Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kufanya majaribio ya utafiti wa jiosayansi kwa kutumia njia ya High Resolution Airborne Geophysical Survey kwa kurusha ndege nyuki angani ili kupata taarifa sahihi za jiolojia ya miamba na udongo katika kijiji cha Masabi wilaya ya kahama mkoani Shinyanga na Kata ya Katente wilaya ya Bukombe mkoani Geita kwa kushirikiana na kampuni ya EllygreenTech.

 

Kama inavyofahamika kuwa, uti wa mgongo wa Sekta ya Madini ni utafiti, Katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa kwa kasi na kuchangia zaidi kwenye uchumi wa nchini, GST imejikita kufanya tafiti za kina kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo urushaji wa ndege. 


Kaimu Mkurugenzi wa Kanzidata ya Taifa ya Rasilimali Madini Bi. Hafsa Maulid akizungumza katika eneo la majaribio ya utafiti amesema GST imejipanga kikamilifu kutekeleza Vision ya 2030 kwa vitendo ambapo itaendelea kufanya tafiti za kina kwa njia ya High Resolution Airborne Survey nchi nzima ili ifikapo 2030 angalau iwe imefikia asilimia 50.


“Tukishafanikiwa zoezi hili, itaongeza taarifa Sahihi za jiosayansi kwa lengo la kuwawezesha wawekezaji kupata taarifa zenye uhakika, pia itasaidia Serikali katika sekta zingine kama Kilimo, Maji na kadhalika kupata taarifa sahihi”, amesema Bi Maulid. 


Aidha, Bi Maulid ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali kwa ubunifu wao, usimamizi, miongozo na maelekezo mazuri wanayoyatoa katika kuiendeleza Sekta ya Madini ambapo mpaka sasa Kampuni ya Ellygreentech tayari imefanya jaribio la kurusha Ndege Nyuki angani katika mkoa wa Dodoma.



Comments