Vijana wakazi wa kata ya Lyambamgongo wilaya ya Bukombe wakimenya karanga tayari kwenda sokoni
"Na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli, Kama mnataka
mali, mtayapata shambani"
Aidha, shairi
hilo hushamirishwa na methali ya Kiswahili isemayo "Jembe halimtupi mkulima." Ikiwa na
maana kwamba mtu yeyote anayeshika jembe na kwenda shambani kulima lazima
atapata chochote kitu.
Wapo ambao kwao mashairi na methali hazikubaki hadithi tamu
za shule bali darasa la mafanikio kama ilivyo kwa Pius Vasco kutoka kata ya
Lyambamgongo wilaya ya Bukombe, Geita.
Katika Makala haya, tunamwangazia mkulima Pius Vasco.
Ambatana nasi!
Bukombe Sasa ilipofika nyumbani kwa Pius ilikuwa majira ya saa 6:00 mchana siku ya Alhamisi Novemba 16, 2023 ambapo ilipokelewa na mkewe Vicky Manyabuluba pamoja na watoto waliokuwa wakisaga karanga kwa ajili ya maandalizi ya mlo wa mchana.
Kabla ya
kujitambulisha kwanza nilishangazwa na kiwango cha utajiri nilichokiona pale
ikiwemo nyumba ya kisasa yenye
umeme, mifumo ya mawasiliano, maji na sura zenye afya na hivyo kuuliza..
"hapa ni kwa Pius Vasco?" Nikujibiwa "Ndiyo" Nikauliza tena
"anafanyakazi gani?" Nikajibiwa " hana kazi, yupo tu.
Nimkulima"
Hata hivyo,Vicky alinihakikishia kuwa Pius Vasco
asingechelewa kufika nyumbani kwani alikuwa tayari amempigia simu kumjulisha
ujio wangu na Pius anamiliki usafiri (chombo cha moto) pikipiki na mashamba
yake hayapo umbali mrefu hivyo nivute subira.
Wakati namsubiri
Pius huku Vicky akiendelea kusaga karanga, kichwani kauli ya "hana kazi,
ni mkulima tu" inanisumbua. Jakaya Kikwete naye ni mkulima mzuri tu,
Mizengo Pinda, Mjwahuzi Karushaija, Masanja Mkandamizaji "lakini hawa
uenda walipata mitaji mikubwa. Lakini Jesse Robert mbona alianza bila mtaji
wowote zaidi ya ardhi na jembe?"
Ghafla kijana wa
miaka 41 baba wa watoto saba aliyehitimu darasa la saba 1998, mpole mwenye
rangi ya maji ya kunde, Pius Vasco anafika ambapo namuuliza kama anafahamu kuwa
Novemba kila mwaka huadhimishwa kama
mwezi wa karanga duniani?
Mkulima wa karanga Pius Vasco kutoka kata ya Lyambamgongo wilaya ya Bukombe Geita akiwa amepumzika nyumnai kwake na familia baada ya kutoka shambani huku mkewe Vicky akisaga karaga kwa lengo la kuandaa mboga ya chakula cha mchana kwa familia hiyo
Pius anakiri kuwa alianza kulima karanga kisasa kwa mbegu bora katika kipindi cha Mbunge Doto Biteko na utawala wa Said Nkumba wilayani humo baada ya wataalamu kufika kijijini hapo na kuanza kupokea mbegu bora kutoka kituo cha Naliendele.
Aidha, alieleza
kupatiwa msaada wa malezi shambani na Afisa Kilimo wa kata ya Lyambamgongo,
Lydia Mtindo na hata kuweza kuunda kikundi cha wakulima 10 ambapo kati yao
wanawake ni wane. Lengo la kikundi hicho ni kuwezesha kufikiwa kirahisi na
wataalamu pamoja na kutoa hamasa kwa wanakijiji wengine kuweza kulima kisasa.
Anataja faida za
kikundi hicho kuwa ni pamoja na kusaidiana wakati wa kupanda, kukumbushana
wakati sahihi wa kupanda na kuvutia mitaji.
"Usione tunapata faida, kuna kazi kubwa kwenye
kupanda. Kutoka shimo moja hadi lingine unatakiwa uache sentimita 10 na mstari
hadi mstari ni sentimita 50. Hivyo utaona ilivyokazi kupanda ekari moja na
zaidi peke yako." alisema Pius
Aliongeza kuwa
baada ya kuacha kilimo cha mazoea na kuanza kulima kufuata ushauri wa wataalam
kumekuwa na ongezeko la mavuno na kipato jambo lililomwezesha kujenga nyumba
zaidi ya moja, kununua pikipiki na kukidhi mahitaji ya familia ikiwemo lishe,
matibabu na shule.
“Baada ya kupatiwa
mafunzo na mbegu bora kutoka Naliendele, eneo ambalo awali niliweza kuvuna
gunia 15 sasa hivi navuna hadi gunia 30 eneo hilohilo” alifafanua
Gunia moja la karanga huuzwa kati ya shilingi 65,000 hadi 100,000 kutegemea na msimu. Alisema wateja wao wakubwa ni kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na wenyeji wa Tanzania kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga ukiacha soko la ndani ya wilaya ambao ununua kwa matumizi ya chakula.
Mwanakikundi,
Edson Hamphrey alilieza Bukombe Sasa kuwa mbali na kuuza karanga ghafi, amekuwa
akijipatia pia mafuta ya kupikia kutokana na zao hilo.
“Huwa namenya
naziosha, nasaga, nakamua mafuta. Katika gunia moja Napata hadi lita 25 za
mafuta. Mafuta ya karanga ni bora kuliko mafuta mengine” alisimua Hamphrey
Hamphrey ambaye awali aliishi eneo la Pasians Jijiji Mwanza
akijishughulisha na biashara ndogondogo (umachinga) baada ya kutoka nyumbani
kwao Singida kutafuta maisha, anasema aliamua kwenda wilayani Bukombe baada ya
kuelezwa na marafiki zake juu ya fursa zilizomo katika wilaya hiyo ikiwa ni
baada ya utawala Mashishanga kuzuia biashara holela mkoani Mwanza.
Kwa upande wake
Elizabeth Hosea ambaye pia Mwenyekiti wa mtaa wa Lyambamgongo alisema kuwa
aliamua kujiunga na kikundi kutokana na faida anazoziona kwa wengine wanaolima
kwa kufuata ushauri wa wataalam.
“Kilimo kimeniwezesha kusomesha watoto na pia kuanzisha
ujasiliamali mwingine mdogo mdogo kama unavyoona pale (anaonesha grocery yake)
na pia nafuga na kuku” alieleza faida Elizabeth akiwa kwenye shamba lake karibu
na barabara kuu ya Rusumo-Kahama aliloliita shamba darasa.
Mwalimu Moses
Nyahiti ambaye amejiingiza kwenye kilimo baada ya kustaafu utumishi wa umma,
alisema kuwa kilimo kimemuwezesha kuendelea kuishi kama ambavyo ilikuwa wakati
akiwa kazini.
“Kwenye kilimo
napata kipato kizuri hususani kwenye karanga. Nyie mnaita maokoto? Kwenye
kilimo maokoto yapo” alieza Mwalimu Nyahiti huku akitabasamu
Aprili 2023, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Said Nkuba
alijitolea kuhamasisha ulimaji wa karanga katika wilaya hiyo baada ya yeye
mwenyewe kulima na kuona faida yake kiuchumi.
Nkumba alitoa ahadi hiyo alipotembelewa na watafiti
wa Zao la Karanga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI kituo cha
Naliendele ambao walifika wilani humo kuona majaribio ya mbegu ya zao hilo.
Alisema kuwa wilaya hiyo ina ardhi nzuri yenye
rutuba hivyo inafaa kwa kilimo cha karanga kwakuwa karanga hazihitaji mbolea
wala viwatilifu na kuagiza wakulima kupatiwa elimu ili waweza kuzalisha zaidi.
“Niko tayari kufanya uhamasisha wa zao la karanga
katika wilaya yangu ili kuwezezsha wakulima kulima kwa wingi zaidi"
“Nitawaunga mkono pale mtakapo hitaji uwepo wangu
kwakuwa mimi ni mkulima mzuri wa zao hili. Napata pesa nyingi kwa kulima
karanga. Wakulima wanaweza kubadili hali
zao kupitia karanga ” alisema Nkumba
Kwa upande wake Afisa Kilimo kata ya Lyambamgongo,
Lydia Mitindo alisema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wakulima wa kata
hiyo kulima kisasa baada ya kuona faida ambazo wengine wanapata kutokana na
kilimo hicho.
“Tumeamua kuanzisha kikundi ili kukitumia kama
darasa pamoja na kuwavuta wenzao japo changamoto ni watu kukubali kubadilika
kwa haraka" alisema Lydia.
Afisa Kilimo kata ya Lyambamgongo, Lydia Mitindo akiwa shambani tayari kutoa ushauri kwa wakulima wa kata hiyo
Mbali na
faida za kibiashara, karanga hutoa mchango mkubwa katika kuboresha afya ya
binadamu.
Kwa mujibu wa taasisi ya chakula na dawa ya Marekani
USDA, karanga ina utajiri wa protini, mafuta mazuri, nishati, nyuzi lishe,
madini chuma, calcium, magnesium, potassium, zinc na phosphorus
Pia inaelezwa kuwa karanga huwa na kampaundi za
resveratrol ambazo huongeza ubora wa afya ya uzazi kwa wanaume pamoja na uwezo
wa kuongeza kiasi cha mafuta mazuri mwilini ambayo huwa na faida kwenye afya ya
moyo.
Novemba kila mwaka huadhimishwa kama mwezi wa
Wapenda karanga duniani. Watu wengi dunia huita mwezi huu kuwa mwezi wa Wazimu
wa Siagi ya Karanga!
Historia ya Mwezi wa Siagi ya Karanga huambana na
historia nzima ya siagi yenyewe na kuenea kwa karanga duniani.
Karanga ni jamii ya kunde ambayo asili yake ni
Amerika Kusini, na imekuwepo duniani kwa takribani miaka 7600.
Ingawa asili ya kitu kama siagi ya karanga inaweza
kufuatiliwa hadi kwa Waazteki na Wainka, historia
yake ya kisasa
inaonekana ilianza mnamo 1884, wakati ilipewa hati miliki na Mkemia wa
Kimarekani anayejulikana kwa jina la Edson.
Madhumuni yake yote ya kuikuza ilikuwa ni kuhakikisha
kwamba wale ambao walikuwa na matatizo ya kutafuna vyakula vigumu wangeweza
kuwa na njia ya ladha ya kupata lishe
waliyohitaji. Hivyo, siagi ya karanga ilizaliwa.
Tangu wakati huo, tiba hii ya ladha na lishe
imelipuka hadi kwenye eneo la upishi katika kila ruhusa inayowezekana na
inaweza kupatikana kwa tofauti fulani katika aina fulani katika milo tofauti
tofauti.
Mnamo 1995, Mwezi wa Wapenda Siagi ya Karanga
ulianza na umekuwa ukiadhimishwa tangu wakati huo katika tamasha la mwezi mzima
la siagi ya karanga!
Jinsi ya kuadhimisha Mwezi wa Wapenda Siagi ya
Karanga ili kwenda sawa na Mwezi wa Wapenda Siagi ya Karanga.
Fanya hivi!
Soma tena faida zitokanazo na karanga ili kupata
manufaa zaidi ya siku 30 nzima za kusherehekea na kufurahia kila kitu kinachohusiana
na siagi ya karanga.
Pika kwa Siagi ya Karanga Kwa kuzingatia jinsi siagi
ya karanga inavyonyumbulika kama kiungo, Mwezi wa Wapenda Siagi ya Karanga ni
fursa nzuri ya kuanza kuweka mboga hii ya jamii ya kunde katika vyakula na milo
mbalimbali.
Kila siku weka
lengo la kuongeza mlo mmoja wenye mada ya siagi ya karanga kwenye menyu ya
kiamsha kinywa, chakula cha mchana au cha jioni.
Pius Vasco
anatoa wito kwa serikali kuwawezesha mikopo yenye riba nafuu ili kuongeza
uzalizaji wa zao hilo.
Shughuli
za uchumi katika wilaya ya Bukombe ni Kilimo na ufugaji ambazo zinachukua asilimia
84 ya Mapato ya wakazi wote wa wilaya hiyo na asilimia 16 inahusisha shughuli
za uchimbaji wa madini,biashara na,ufugaji nyuki.
Ikiwa
ni kati ya Halmashauri sita zinazounda
Mkoa wa Geita, halmashauri hii inaushawishi wa kutosha kuweza kukumbuka
shairi la “Karudi Baba Mmoja” kutokana na kuzungukwa na misitu kwa asilimia 60 na
asilimia 40 ya eneo lote kufaa kwa makazi, Kilimo na Ufugaji.
Comments
Post a Comment