Wanawake wilayani Bukombe wapewa mbinu za kilimo bora

 ·       Lengo ni kuboresha lishe, mapato na usawa wa kijinsia

·       Wanawake wa wilaya hiyo wajivunia ongezeko la mavuno

·       DED awataka maafisa ugani kuongoza hamasa vijijini

Sehemu ya baadhi ya wanawake wa wilayani Bukombe wakisikiliza mkufunzi katika mafunzo ya kilimo cha kisasa na usawa wa kijinsia yaliyofanyika hivi karibuni ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mwanamke wa kijijini.

Siku ya Oktoba 15 ya kila mwaka Tanzania huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mwanamke anayeishi Kijijini kwa kumpatia mbinu mbalimbali za kujikwamua katika maisha na kuhimiza usawa wa kijinsia katika jamii.


Mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika kitaifa Kijiji cha Levolos, kata ya Kimnyaki mkoani Arusha ambapo yaliambatana na maonesho ya siku mbili kuanzia tarehe 14 hadi 15 Octoba 2023 ambapo TWCC kwa kushirikiana na Shirika la Umoja Mataifa linaloshughulikia masuala ya Usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake (UN Women) ilifadhili wanawake wajasiriamali wa vijjini watano kushiriki kupitia Kupitia "Mradi wa pamoja wa kuongeza kasi ya uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Vijijini (Mwanamke Na Uchumi)"


Kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Watoto Dkt. Dorothy Gwajina maadhimisho yalienda sambamba na Mafunzo na Mdahalo juu ya masuala ya Jinsia, Ukatili wa kijinsia, masuala ya Haki za Ardhi na mabadiliko ya Tabia nchi, Malezi na Ustawi wa Afya, Usalama wa Chakula na Mpango wa Matumizi ya Ardhi.


Maadhimisho hayo ni kufuatia Tamko la Umoja wa Mataifa na Azimio Namba 62 la Tarehe 18 Disemba, 2007.


Azimio hilo lilitambua Oktoba 15 ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Wanaoishi Vijijini na kuzitaka Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku hiyo.


Siku hiyo imeanza kuadhimishwa Kimataifa kwa mara ya kwanza tarehe 15 Oktoba, 2018.


Lengo la Maadhimisho ni kutambua na kuuenzi mchango wa wanawake wanaoishi vijijini hususan katika nyanja zauzalishaji wa mazao ya Kilimo, kuhakikisha Usalama wa Chakula Kaya na kuchangia Ukuaji wa Uchumi wa Taifa.


Wilayani Bukombe, Maadhimisho yalifanyika katika viwanja vya Runzewe Kaulimbiu ikiwa ni “Wezesha Wanawake wanaoishi kijijini kwa uhakika wa chakula, lishe na uendelevu wa familia”


Afisa Maendeleo Wilaya ya Bukombe, Benadetha Tehingisa alisema kuwa ya siku ya kilele Octoba 15 ilitanguliwa na matukio kadhaa yaliyoandaliwa na wilaya hiyo kwa wanawake wanaoishi kijijini ikiwemo semina dhidi ya ukatili wa kijinsia, kilimo bora na jinsi ya kujikwamua kiuchumi lengo likiwa ni kuleta usawa wa kijinsia katika jamii.


“Tumefanya semina katika ngazi ya kata kwa kushirikiana na wataalamu wetu na tulenga kumjengea uwezo mwanamke wa kijijini amabaye kimsingi bado anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa jinsia. Lakini pia wanaume hatukuwabua katika mafunzo hayo. ” Alisema Benadetha

Afisa kilimo Kata ya Runzewe Mashariki, Hillary Munyuku akitoa elimu na mbinu za kilimo bora kwa wanawake wa kata hiyo

Kaulimbiu inasisitiza umuhimu na nafasi kubwa ya Wanawake wanaoishi vijijini katika kushughulikia ustawi wa familia ikiwemo ushiriki wao katika kilimo ili kuboresha lishe ya familia katika jitihada za kukabiliana na utapiamula na udumavu kwa watoto


Njaa na matumizi mabaya ya ardhi ni kati ya mambo amabyo yanaongeza ugumu wa maisha kwa wanawake wanaoishi vijijini.


Akieleza matumizi sahihi ya ardhi na mbinu ambazo amewapa wanawake wanaoishi kijijini Afisa Kilimo Kata ya Runzewe Mashariki, Hillary Munyuku alisema ni pamoja na hatua zinazotakiwa kuachwa kati ya mche na mche, tuta na tuta wakati wa kupanda, matumizi sahihi ya mbolea na dawa, na wakati sahihi wa kuanza kuaandaa shamba”


“Kabla ya kuwapatia mafunzo, baadhi ya wakulima walikuwa wakipata mavuno kidogo ukilinganisha na sasa. Hii ni kwasababu wengi ilikuta ameeacha hatua 100/40 badala ya 70/30 na hivyo kuishia kulima mbuga. Lakini katika eneo dogo mkulima anavuta hata mara mbili ya alivyovuna mwanzo” Alisema Munyuku

Mkulima anayejulikana kwa jina la Boss Msonga akiwa anawajibika shambani Bukombe

Mkulima Agnes John wa Kijiji cha Mwamakunkwa Kata ya Iyogelo ililieleza gazeti hili faida za mafunzo yanayotolewa na maafisa kilimo kuwa ni pamoja na ongezeko la mavuno.


 “Tunapewa mbinu za kulima na kupanda kisasa mbegu zilizobora tofauti na zamani ambapo tulinunua tu mahindi sokoni na kutupia shambani huku shamba moja tukiwa tunachanganya na mahindi, karanga, kunde na mihogo humohumo” alisema Agnes akifurahia mavuno ambayo ameanza kuyapata kutokana na jitihada za halmashauri ya Bukombe





Afisa Kilimo akifurahia jambo pamoja na wakulima wakati wa maandalizi ya shamba kabla ya kupanda

Katika kuhakikisha Kauli Mbiu ya mwaka huu inatekezwa kwa vitendo na wananchi wa wilaya ya Bukombe wanamudu mahitaji ya kaya ya milo mitatu kwa siku, Mkurugenzi wa wilaya hiyo Lutengano Mwalwiba aliwataka maafisa kilimo, mifugo na uvuvi wa wilaya hiyo kuanzia ngazi za vijiji na kata kuongeza ubunifu katika maeneo yao ya kazi na kuaanda mpango wa kushirikiana na wakulima kuongeza uzalishaji.


 Akizungumza na watumishi hao katika ukumbi wa halmashauri Siku ya Alhamisi Octoba 19, 2023, Mwalwiba alisema wilaya inawategemea katika kuboresha maisha ya wakulima, wafugaji na bidhaa za uvuvi na kuongeza mapato ya halmashauri hiyo!

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Lutengano Mwalwiba akizungumza na maafisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Vijiji na Kata katika ukumbi wa halmashauri hiyo Octoba 19, 2023

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,  Zedekia Solomoni aliwataka maafisa ugani kuhakikisha wanawahamasisha pia kilimo cha pamba ili kila kaya ilime angalau hekari mbili.


 “Ardhi, au tuseme kilimo ni nyenzo muhimu kwa Maendeleo ya Mwanamke wa Kijijini. Asilimia 80 ya watu wote wanaishi kijijini na wanawake ni wengi ambao tunaamini ndiyo wazalishaji wakuu wa chakula”. Anaeleza Mkurugenzi wa Sauti ya Wanawake Ukrewe, Sophia Donald


Sophia alifafanua kuwa mchango wa mwanamke wa kijiji unaweza kusionekane moja kwa moja kutokana na mila na tamaduni zinazomzunguka.


Alitoa rai kwa maadhimisho hayo kutumika kuibua mjadala wa wadau mbalimbali kiwemo Serikali kuweka mazingira mazuri ya umiliki wa ardhi kwa mwanamke wa kijijini kiwemo marekebisho kwenye sharia ya mirathi.


“Mwanamke akiwa na uhakika wa ardhi kunamuongezea uhakika wa chakula cha kutosha pamoja na uhakika wa kipato na hivyo kupunguza ukali wa matendo ya ukatili kwa kukosa maamuzi dhidi ya kile wanachozalisha” alisema Mkurugenzi huyo wa Sauti ya Wanawake Ukerewe, Sofia

Mkurugenzi wa shirika la Sauti ya Wanawake Ukrewe (SAWAU), Sophia Donald

 Wakati umaskini kwa ngazi ya ulimwengu ikielezwa kupungua kwa kiasi Fulani, bado watu wengi wanaendelea kuishi katika hali za umaskini wa kukithiri hasa katika maeneno ya vijijini japokuwa ndiko hutegemewa zaidi kwa uzalishaji wa kilimo wa karibia asilimia 80 za chakula barani Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuwezesha kusaidia watu wengi wakiwemo wa mijini.


Afisa Maendeleo ya Jamii, Anna Athanas alieleza hali ilivyo katika jamii kuwa katika sekta ya kilimo, wanawake wanaweza kuwa na tija na biashara kama wenzao wa kiume, lakini wana ufikiaji mdogo wa ardhi, mikopo, masoko na kupata bei ya chini kwa bidhaa zao.


Aidha, inaelezwa kuwa vizuizi vya kimuundo na kanuni za kijamii bado ni za kibaguzi na zinaendelea kupunguza jukumu la wanawake katika familia na jamii za vijijini.


“Wanawake na wasichana hawana ufikiaji sawa wa rasilimali na bidhaa, huduma za umma kama elimu, huduma za afya na miundombinu, na kazi zao nyingi hazionekani na hazilipwi” yananukuliwa baadhi ya machapisho mtandaoni.


Kwa ngazi ya Ulimwenguni, isipokuwa chache, viashiria vyote vya jinsia na maendeleo ambavyo takwimu zinapatikana zinaonesha kuwa wanawake katika maeneo ya vijijini wanaishi bila usawa katika hali ya umaskini, kutengwa na wanaathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi kuliko wanaume.


 Mabadiliko ya tabianchi huathiri ustawi wa wanawake na wanaume kwa njia tofauti katika suala la uzalishaji wa kilimo, usalama wa chakula, afya. Ripoti kadhaa zimeeleza kuwa katika maeneo ya vijijini mara nyingi wanawake ndio wa kwanza kuhathirika uharibifu wa maliasili na kilimo.


Wanawake vijijini wanapaswa kupewa mbinu mpya za kulima kisasa ili kuboresha lishe kwa kuhakikisha milo mitatu katika ngazi ya Kaya, kwa ajili ya lishe bora ya familia na baadaye kuweza kuuza ziada na kuboresha kipato. Wanawake vijana wanahitaji kupata pembejeo za kilimo ili waweze kulima kadiri inavyowezekana.


Mbunge wa jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Tanzania, Dkt. Doto Biteko amekuwa akishirikiana na wananchi pamoja na viongozi wa jimbo hilo kuhakikisha ufanisi na uwezeshaji wa sekta zote muhimu katika kuboresha maisha ya wakazi wa jimboni wakiwemo wanawake na watoto kupitia huduma mbalimbali ikiwemo ubora wa lishe, elimu, maji na miundombinu ya afya na barabara


Comments