Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) uanze mapema ili Watanzania wapate umeme wa uhakika.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2023 alipokutana
na kufanya kikao na ujumbe wa Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi
kutoka nchini Misri, Mhe. Dkt. Assem Elgazzar kuhusu maendeleo ya utekelezaji
wa mradi wa JNHPP jijini Dar es Salaam.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais Samia ana mategemeo makubwa
kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo na anatamani mwanzoni mwa mwaka 2024
utekelezaji wake uanze na kuongeza kuwa mradi wa JNHPP ndio mwarobaini wa
kutatua changamoto ya hali ya upatikanaji wa umeme nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya
Makazi, Dkt. Elgazzar ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiamini nchi hiyo
katika kutekeleza mradi huo. Pia amesema mradi huo utakua wa mfano katika
ufuaji wa umeme.
Naye, Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mhe. Sherif Ismail
ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji
wa miradi mbalimbali ikiwemo wa Bwawa la kufua umeme la JNHPP.
Kikao hicho kilihudhuriwa na ujumbe wa TANESCO, Kampuni
inayotekeleza mradi wa JNHPP (Elsewedy Electric na Arab Contractors) ya nchini
Misri na Wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati
Comments
Post a Comment