WAZIRI BITEKO ASHUHUDIA MAKUBALIANO KATI YA STAMICO NA CRDB




  


Ikiwa ni mwanzoni kabisa mwa mwaka 2022, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko  ameshuhudia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na Benki ya CRDB  wakitiliana saini Makubaliano ya Awali ya Kuwasaidia Wachimbaji Wadogo Kupata Mikopo.





Tukio hilo limefanyika wakati wa Mkutano  Mkuu  wa 24 wa  Chama cha Wachimbaji Wanawake Tanzania (TAWOMA) uliofanyika jijini Dodoma.



Akizungumza wakati akifungua Mkutano huo, Waziri wa Madini  Dkt. Biteko amezipongeza taasisi hizo  STAMICO na Benki ya CRDB  zikiwemo  taasisi nyingine za  fedha kwa kubadilisha mtazamo dhidi ya wachimbaji wadogo na kuamua kuwakopesha.


Amesema STAMICO ina jukumu kubwa la kuthibitisha taarifa za jiolojia za wachimbaji wadogo kwa kuwa daraja kwa wachimbaji wadogo katika kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha.


Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wanachama wa TAWOMA na kuwataka kuwa vinara katika sekta ya madini ili kuondoa dhana ya unyonge wanapokuwa katika kazi zao katika mnyororo wa uchimbaji madini.


Amesema wanawake ni hazina kubwa kwa Taifa kwa kuwa wana uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja kwa wakati mmoja, wana kiwango kikubwa cha uaminifu na kwamba wanawake wakishirikishwa vizuri katika mnyororo wa uchimbaji madini itainufaisha jamii nzima ya Watanzania.


Amewataka wanawake hao kutosahau jukumu lao la malezi kwa familia zao wakati wanatekeleza shughuli za uchimbaji ili kuweza kujenga jamii yenye tabia nzuri na kukubalika katika jamii. Pia, amewataka

 kukemea tabia ya kulalamika na badala yake kuwajenga katika kujituma na kujisimamia.


Akzungumza kama Mlezi wa Wachimbaji Wadogo,  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse ameishukuru Benki ya CRDB kwa kukubali kuwasaidia Wachimbaji Wadogo  kupata mikopo ambayo imekuwa  kilio kikubwa cha muda mrefu kwa Wachimbaji Wadogo.


Ametoa pongezi kwa wanawake wachimbaji (TAWOMA)  na kuwekeza kuwa wana nguvu ya uthubutu, ubunifu na ujasiri wa kujikita katika sekta hiyo ya uchimbaji mdogo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiaminika ni maalum kwa ajili ya wanaume tu.


“Niliwahi kukaa na kina mama wa TAWOMA wakanielezea mikakati yao, kwa kweli kina mama hawa wana maono ya mbali sana”. 


Ameahidi kuwa, STAMICO itakuwa na wachimbaji hao bega kwa bega ili kuhakikisha wanafikia malengo yao kwa kutokana na namna wanavyopambana wanapambana licha ya vikwazo mbalimbali wanavyokutana navyo katika utekelezaji wa majukumu yao.


Amewataka wachimbaji wadogo hususani wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokea zikiwemo za biashara ya mkaa mbadala wa rafiki Briquette ambao utazalishwa na STAMICO, kushiriki katika mafunzo, maonesho ya kibiashara na kuhakikisha wanashiriki pia katika maonesho ya kimataifa kwa kuwa kazi zao nyingi zinaonekana kupendwa hata nje ya nchi.


Akizungumza kwa niaba ya  Mkurugenzi Mkuu wa CRDB   Bw. Prosper Nambaya  amesema CRDB imeamua kuingia katika sekta ya uchimbaji kwa kutumia utaratibu maalum utakaokubalika kati yao, STAMICO na wachimbaji ili kuhakikisha kila pande inanufaika kutokana na makubaliano hayo ikiwemo  ujasiri walioupata kupitia mikopo mbalimbali ambayo wamewahi kuitoa kwa taasisi nyingine.


Ameongeza kuwa, makubaliano hayo ni mwanzo kuleta ukombozi kwa wachimbaji wadogo na kwamba yanakwenda kutekeleza kwa vitendo ili kuleta tija katika sekta ya uchimbaji mdogo.


Aidha , kwa niaba ya wanawake wachimbaji wa madini (TAWOMA) Bi. Salma Ernest ameishukuru STAMICO kwa kuwa Mlezi kwa vitendo, kwa kuwa hadi sasa wameweza kushirikiana katika vitu vingi na kuhakikisha chama kinasimama imara na elimu ya uchimbaji inawanufaisha wanachama wote.


Amesema malengo ya chama hicho ni pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha madini yanaongezewa thamani ndani ya nchi, wanawaweka pamoja wachimbaji ili kuhakikiksha wananufaika na fursa za mikopo zinayotolewa na mafunzo mbalimbali.


STAMICO inaendelea kufungua fursa kwa wachimbaji wadogo ili kuhakikisha sekta hii inakua kwa kiasi kikubwa na kuleta tija kwa Taifa.

Comments