SERIKALI YAINGIA MAKUBALIANO KUCHIMBA MADINI YA NICKEL KABANGA










Imeelezwa kuwa mkoa wa Kagera upo katika ukanda unaopatikana madini ya Nickel na Bati hivyo ili nchi iweze kunufaika na madini hayo, Serikali imeamua kuingia makubaliano na Kampuni ya LZ Nickel Limited na makubaliano hayo yanalenga kuunda ubia utakaokuwa chini ya Kampuni ya pamoja ijulikanayo kama Tembo Nickel Corporation Limited.




Hayo yameelezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jonh Pombe Magufuli ailipokuwa kwenye Hafla ya Utiaji Saini wa Mkata kati ya Serikali ya Jamhuli ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya LZ Nickel Limited ya nchini Uingereza.




Rais Magufuli amesema ikumbukwe kuwa madini ya nickel katika eneo la Kabanga wilaya ya Ngara mkoani Kagera yaligunduliwa mwaka 1976 na utafiti wa kina wa madini ya nickeli na madini mengine katika eneo hilo ulianza toka miaka ya 2000 na kugundulika kuwa nickel iliyopo eneo hilo ni daraja la kwanza na ni madini bora duniani.



“Nimetaarifiwa kuwa kutokana na utafiti wa madini ya nickel katika eneo la Kabanga, mashapo yapatayo takribani tani milioni 51.73 za madini ya nickel zimegundulika ambazo zitachimbwa kwa miaka 32 na ukubwa wa eneo la mradi ni kilometa za mraba 201.85 ambapo Kabanga ndiyo eneo lenye madini mengi zaidi duniani, huu ni mradi mkubwa sana,” alisema Rais Magufuli.




“Ni azma ya Serikali kuona kuwa nchi ya Tanzania inanufaika na madini yake na pia kuona wawekezaji wanapata manufaa kwa kuwekeza nchini. Kupitia mradi  huo Serikali itapata manufaa mbalimbali kupitia Kodi, Tozo, ajira, huduma kwa jamii na ununuzi wa bidhaa na huduma zinazopatikana hapa nchini. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na uchakataji wa madini zinasimamiwa vizuri ili tuweze kunufaika na madini yetu,” aliongeza Rais Magufuli.



Kwa upande wake Waziri wa Madini Doto Biteko amempongeza Rais Magufuli kukubali kuja kushuhudia hafla hiyo ya kutiliana Saini makubaliano ya kuendesha uchimbaji wa madini ya Nickel kwa ubia na Kampuni ya LZ Nickel Limited na pia amemshukuru kwa miongozo ambayo umekuwa ukiwapatia katika kusimamia Sekta Madini.




“Naomba kutoa pongezi za kipekee kwa Timu yetu ya Majadiliano kwa kufanikisha majadiliano kwa ufanisi mkubwa na uzalendo wa hali ya juu katika Sekta ya Madini hasa katika madini ya kimkakati kama Nickel.




Ninatambua kazi hii ilikuwa ngumu na yenye jasho jingi lakini mlijitoa kwa dhati hadi kufanikisha na leo hatimaye tunafungua ukurasa mpya,” alisema Waziri Biteko.




Aidha, Waziri Biteko amesema kuwa, Sekta ya Madini imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa mathalan Mwaka 2019 Sekta ya Madini imekuwa kwa asilimia 17.7 na kuongoza katika ukuaji ukilinganisha na sekta zingine hapa nchini ambapo mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019. 



Pia sekta ya madini ndio inaongoza kwa sasa tangu mwaka 2020 kwa kuingizia nchi yetu fedha za kigeni na imeendelea kuimarika hata katika kipindi chote cha janga la korona.




“Hivyo, ni matarajio yetu kuwa, Sekta ya Madini itazidi kukua na kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa na kuwanufaisha wananchi waliopo katika maeneo yanakopatikana madini kama ilivyo kwa madini ya Nickel ya Kabanga, unaamini kuwa hadi kufikia Mwaka 2025 mchango wa sekta hii utafikia asilimia 10 katika pato la Taifa kama inavyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo,” aliongeza Waziri Biteko.




Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, amesema katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda kutokana na rasilimali madini, Serikali kupitia Wizara ya Madini ilikaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika tasnia ya uyeyushaji (smelting) na usafishaji (refining) madini ili shughuli hizi ziweze kufanyika nchini ambapo hadi sasa, Serikali imetoa leseni nne (4) za usafishaji (refinery) na leseni sita (6) za uyeyushaji (Smelting).

Comments