Virusi vya corona: Utafiti wabaini Wakenya karibu milioni 2.6 wameugua Covid-19

Kupimwa kwa antibodies kumeonesha kuwa Wakenya wengi tayari wamepata maambukizi kuliko ilivyokuwa ikibainika katika shughuli za upimaji nchini humo, kulingana na Kemri
Maelezo ya picha,

Kupimwa kwa antibodies kumeonesha kuwa Wakenya wengi tayari wamepata maambukizi kuliko ilivyokuwa ikibainika katika shughuli za upimaji nchini humo, kulingana na Kemri

Karibu Wakenya milioni 2.6 tayari wana virusi vya corona, wanasayansi wameeleza baada ya kupima damu iliyotolewa kwa ajili ya protini inayotumika kwenye mfumo kinga.

Protini hiyo (antibody) hutengenezwa na mwili kwa ajili ya kushambulia virusi na bakteria, na uwepo wake kwenye damu unaashiria kuwa mtu huyo hakuwahi kuwa na maambukizi- hata kama mtu huyo hakuwahi kuonesha dalili.

Watafiti kutoka Taasisi ya utafiti wa tiba nchini Kenya wameunga mkono mfuko wa kuchangia damu uliofanyika nchi nzima kati ya mwezi Aprili tarehe 30 na tarehe 16 Juni.

''Kupimwa kwa antibodies kumeonesha kuwa Wakenya wengi tayari wamepata maambukizi kuliko ilivyokuwa ikibainika katika shughuli za upimaji nchini humo.,'' Ilieleza taasisi ya Kemri mapema wiki hii ikinukuliwa nan a gazeti la the Star nchini Kenya.

coronavirus
Maelezo ya picha,

Baadhi ya watu inawezekana waliathirika mapema mwezi Machi kwa kuwa protini hizo zinazopambana na virusi zinaweza kuwa kwenye damu kwa miezi kadhaa, imesema KEMRI

Kemri inakadiria kuwa karibu watu 550,000 jijini Nairobi na karibu 100,000 mjini Mombasa, tayari wameugua virusi hivyo na kupona na pengine kupata kinga.

Imeelezwa kuwa baadhi inawezekana waliathirika mapema mwezi Machi kwa kuwa protini hizo zinazopambana na virusi zinaweza kuwa kwenye damu kwa miezi kadhaa.

Idadi hiyo inaonesha kuwa Wakenya wameshuhudia idadi kubwa ya watu waliopata maambukizi halikadhalika vifo, taasisi hiyo ya utafiti ikikisia kuwa takriban watu 6,000 watakuwa wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchi nzima, kutokana na idadi ya sasa ya vifo nchini humo kwa ujumla.

Kwa mujibu wa gazeti la The Standard media, sehemu ya ripoti ya taasisi ya Kemri ilisomeka kuwa katika mji kama Nairobi kwa mfano, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa wakati utafiti ulipokuwa ukifanyika ni 2,732 ikilinganishwa na idadi ya 550,000 wanaokisiwa kuwa na maambukizi na mjini Mombasa watu 1,368 lakini watu 100,000 wanakisiwa kuwa na maambukizi kutokana na utafiti huo.

''Namna nzuri ya kupima kujua walioambukizwa miongoni mwa raia wa Kenya ni kutembelea maeneo mbalimbali ya makazi kwa ajili ya kukusanya na kupima sampuli za damu''. ''Lakini hili halijaweza kufanikiwa kwasababu ya masharti yaliyopo kutokana na hali ilivyo hivi sasa,'' Ripoti hiyo ilieleza.

Lakini Mkurugenzi wa masomo ya sayansi na teknolojia katika Chuo kikuu cha Nairobi Dkt Ayah amesema kuwa idadi ya sampuli ni ndogo sana kwa majibu yake kutumika kwa raia wote kutathimini mwenendo wa maambukizi ya Covid-19.

CHANZO : bbcswahili.com

Comments