Walimu watatu wa Shule ya Sekondari
Kasamwa, Wilaya ya Geita, mkoani Geita, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi
kwa tuhuma za kumshambulia mwanafunzi wa kike kidato cha tano hadi
kuzirai kwa madai ya kutoga masikio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mpojoli
Mwaburambo, alithibitisha jana kuwapo kwa tukio hilo. Alisema
mwanafunzi huyo Anneth Kulwa (19), baada ya kushambuliwa alikimbizwa
katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa ambako alitibiwa na kupatiwa fomu Na.
3 ya Jeshi la Polisi (PF3).
Kamanda Mwaburambo alisema tukio hilo
lilitokea Desemba 12, majira ya saa 5 asubuhi na chanzo kinadaiwa kuwa
walimu hao kumtuhumu mwanafunzi huyo na wenzake saba kutoga masikio na
kuchukua jukumu la kuwaadhibu.
Alisema baada ya tukio hilo kubainika,
polisi ilifuatilia kwa kuchukua maelezo ya wanafunzi na kufunguliwa
jalada la uchunguzi. Aidha, Kamanda alisema polisi walifika eneo la
tukio na kuwakamata watuhumiwa na kuahidi kuwa uchunguzi utakapokamilika
watafikishwa mahakamani.
Akizungumzia tukio hilo akiwa wodini,
mwanafunzi huyo alisema anakumbuka kabla ya kupoteza fahamu yeye na
wanafunzi wenzake saba walikuwa wakishambuliwa na walimu kwa kipigo cha
viboko, makofi na mateke.
Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, Mkuu
Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kasamwa, Happy Magati, alikiri kutokea
tukio hilo, lakini akadai asingeweza kulizungumzia kwa kina kwa sababu
tayari lilikuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa uchunguzi.
Comments
Post a Comment