Chama
cha Mapinduzi (CCM) kimewaonya watu wanaotumia vibaya mitandao ya
kijamii kuweka habari za uongo zinazowahusu viongozi wa chama hicho
tawala.
Pia, kimesema Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally hana akaunti ya mtandao wa kijamii wa Twitter.
Chama hicho tawala kimetoa taarifa yenye
ufafanuzi huo Jumatano Desemba 5, 2018 ikiwa ni siku moja tangu Dk
Bashiru Ally kukanusha taarifa za mtandaoni zilizomnukuu akimjibu
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole inaeleza kuwa watu
wanaotumia vibaya mitandao ya jamii wana lengo la kuleta taharuki.
“Kuna akaunti ya mtandao wa Twitter yenye jina la Bashiru Ally na inatoa kauli ambazo sio zake,” inaeleza taarifa hiyo.
“Jana katika mitandao ya kijamii watu
wenye hila, fitna, husuda na kila chembe ya uzandiki wametengeneza kauli
ya kubeza, potofu na isiyo na ukweli kuwa Bashiru Ally amemjibu
kiongozi mstaafu, mwanachama wa CCM na kada mwenzetu mzee Pius Msekwa,”
imeongeza.
Mbali na hayo, Polepole amesema kulikuwa
na upotoshwaji wa taarifa za chama hicho iliyodai kuwepo kwa mkutano wa
wanahabari katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba Dar es
Salaam.
“Utaratibu wa CCM msemaji ni mmoja naye
ni mwenyekiti, kwa niaba ya chama anayekasimiwa dhamana ya kusema ni
Katibu wa halmashauri kuu ya Taifa, mwenye dhamana ya itikadi na uenezi
na si vinginevyo,” amesema Polepole.
Polepole amezitaka mamlaka zinazohusika kuchunguza na kuchukua hatua zinazostahili kwa watu wanaotumia vibaya mitandao ya jamii.
Comments
Post a Comment