Mkazi
wa Kijiji cha Mahyolo, Kata ya Nyamihyolo, Wilayani Bunda, Mkoa wa
Mara, Busimba Malegesi amemuokoa mumewe asiuawe na jambazi mwenye silaha
ambaye alivamia katika nyumba yao na kuanza kumshambulia mwanaume huyo
kwa kumkatakata mapanga mwili mzima.
Busimba
alimrukia jambazi huyo kiunoni na kumuangusha chini na kufanikiwa
kumnyang’anya panga pamoja na tochi ambazo alikua nayo wakati
anamshambulia mumewe aitwaye Samson Malegesi (62).
Tukio
hilo la kusikitisha lilitokea saa 7:30 usiku wa kuamkia Ijumaa wakati
familia hiyo ikiwa imelala ndipo jambazi huyo alivunja mlango na kuingia
moja kwa moja chumbani kwa wanandoa hao na kuwasha tochi kumsaka
Malegesi na baada ya kufanikiwa kumuona alianza kumshambulia kwa kumpiga
mapanga kichwani, mikononi, kwenye mbavu na kusababisha damu nyingi
kumwagika.
Wakati
jambazi hilo akiendelea kumshambulia Malegesi, mkewe alikua naye
anapambana kwa kumzuia asimshambulie mumewe, lakini jambazi hilo
lilizidiwa baada ya mwanamke huyo kupata nguvu zaidi na kufanikiwa
kumuangusha chini na kuhakikisha silaha aliyoishika mkononi
akinyang’anywa kwa urahisi kutokana na kubanwa kwa juu na mwanamke huyo.
Mwanamke
huyo wakati akipambana na jambazi huyo alikua akipiga kelele lakini
sauti yake haikuweza kuwafikia majirani ili waweze kumpa msaada, hata
hivyo jambazi huyo baada ya kuona anakosa nguvu baada ya kukandamizwa
chini, akafanikiwa kupata upenyo ndipo akakimbia kutoka katika nyumba
hiyo.
Hata
hivyo, baada ya jambazi huyo kukimbia, mwanamke huyo alitoka nje kuomba
msaada zaidi kwa majirani na walifanikiwa kufika na walimpeleka
Hospitali ya Misheni ya Kibara Wilayani humo ambapo alifikishwa akiwa
hajitambui na kuanza kupewa matibabu ya haraka ili kuokoa maisha yake.
Muuguzi
wa Hospitali hiyo, Godliver Josephat alisema amempokea mgonjwa huyo
akiwa na waaguzi wenzake, saa 9:00 usiku akiwa hajitambui na ndipo
wakashirikiana na madaktari wakamuwekea dawa ya kuzindua uhai wa mgonjwa
huyo na kufanikiwa kuzinduka na wakaendelea na tiba zingine ikiwemo
kuzuia kutoka damu pamoja na kushonwa sehemu alizokatwa mapanga.
“Tumempokea
mgonjwa huyo saa tisa usiku akiwa ana hali mbaya sana, jitihada zetu
zilifanikiwa kumpa huduma ya kwanza kwa kumuwekea dawa ya kuzindua uhai
wake na baadaye tukaendelea kumpa huduma zingine ikiwemo kuanza kumshona
kwasababu alikatwa panga la kichwa, mikono yake yote miwili
ilijeruhiwa, mbavu zake upande wa mgongoni alichimbwa kwa kukatwa na
panga, hivyo hali yake ilikua tete, hata hivyo tumefanikiwa kumuhudumia
kwa umakini mkubwa na sasa mnamuona anaweza kuzungumza,” alisema
Godliver.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ambaye alikua katika ziara
ndani ya jimbo lake ambapo tukio hilo limetokea, mara baada ya kupata
taarifa ya tukio hilo alfajiri ya jana, alifika hospitalini hapo na
kuelekea chumba cha upasuaji akakuta madaktari wakiendelea kumshona
sehemu mbalimbali za mwili wake zilizojeruhiwa.
Lugola
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo la Mwibara, aliwasili Hospitali hapo
akiwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara (OCS), Mkaguzi Boniface
Mwalupale pamoja na madiwani na viongozi wa Halimashauri wa Wilaya ya
Bunda ambao uambatana nao wakati akiwa katika ziara zake jimboni mwake.
“OCS
hakikisheni hamlali mpaka mnalipata jambazi hili kwa kutumia njia zote
za kiintelejinsia mulizosomea ili muweze kumsaka na kumtia mbaroni
haraka iwezekanavyo, huu ni unyama na lazima akamatwe, mtafuteni usiku
na mchana, msikae ofisini kunywa chai, hakikisheni huyu mtuhumiwa
anakamatwa.” Alisema Lugola.
Lugola
baada ya kutoa maelekezo hayo saa mbili asubuhi, alitoka hospitali hapo
na kuendelea na mikutano ya hadhara jimboni humo na akasisitiza kuwa
majambazi wasiibipu serikali kwa kuwa bado ipo macho kuhakikisha
wananchi wake wapo salama, kutokana na tukio hilo Polisi watafanya kazi
usiku na mchana kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa.
“Nampongeza
sana mwanamke aliyepambana na jambazi ili amuokoe mumewe, hakika kama
sio ushujaa wa mwanamke huyo tungempoteza mumewe kwasababu jambazi huyo
alidhamiria kumuua kwa kumkata mapanga zile sehemu ambazo ni hatari
zaidi kwa uhai wa ubinadamu,” alisema Lugola alipokua anazungumza na
wananchi wa Kijiji cha Busagara, Kata ya Chitengule, jimboni humo jana
jioni.
Kwa
upande wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibara, Mwalupale alisema baada ya
kupata taarifa ya tukio hilo, tayari askari wapo katika msako mkali wa
kumsaka jambazi huyo na wamemhakikishia Waziri Lugola pamoja na wananchi
kuwa watamkamata mtuhumiwa huyo.
“Jambazi
huyo alifanya uvamizi huo lakini hakuiba chochote ndani ya nyumba hiyo,
inaonyesha kuwa, lengo la jambazi hilo alitaka kumvamia mtuhumiwa
pekee. Ila tunaendelea kufanya uchunguzi kujua lengo la mtuhumiwa huyo
kufanya tukio hilo la kinyama, na tutahakikisha tunamkamata na
kumfikisha mahakamani,” alisema Mwalupale.
Hata
hivyo, Waziri Lugola baada ya kumaliza mikutano yake jioni alirudi tena
hospitalini hapo na kumkuta mgonjwa huyo ametoka chumba cha upasuaji na
amepelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
Lugola
alitoa pole kwa ndugu na wananchi waliokuwepo hospitalini hapo kutokana
na unyama aliofanyiwa mwananchi huyo na kuhahidi Serikali ipo pamoja
nao na watahakikishia jambazi hilo pamoja na wengine watakamatwa.
Comments
Post a Comment