Msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu leo
amefika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam
kwa ajili ya kusikiliza kesi inayomkabili ambapo anashtakiwa na Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa tuhuma za kuchapisha na kusambaza
video za maudhui ya ngono mitandaoni.
Wema amefika mahakamani hapo majira ya
saa 3 asubuhi akiongozana na mama yake mzazi, Mariam Sepetu na wakili wa
msanii huyo, Reuben Simwanza, na kwenda moja kwa moja hadi kwenye
ukumbi wa mahakama hiyo kusubiri kuanza kusikilizwa kwa kesi yake.
Shauri la kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya
kutajwa katika Maakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya hakimu, Maira
Kasonde huku Wakili wa utetezi akiwa Ruben Simwanza na upande wa Jamhuri
ukisimamiwa na Wakili Jenifer Masue, lakini imeahirishwa hadi Desemba
12 mwaka huu kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Novemba 1, 2018 Wema alipandishwa katika
mahakama hiyo akikabiliwa na shtaka la kusambaza video ya ngono
kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, kesi yenye jalada namba KJN/
RB/13607/2018-KUCHAPISHA NA KUSAMBAZA MAUDHUI YA NGONO MTANDAONI.
Wema alisomewa shtaka hilo mbele ya
Hakimu Mahira Kasonde ambapo alikana kosa hilo kisha kuachiwa kwa
dhamana ya Shilingi milioni 10 kupitia kwa Salim Limu, ambapo Hakimu
aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 20, mwaka huu (jana) ambapo
haikusikilizwa kwa sababu ilikuwa ni Sikukuu ya Maulid.
Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya
Mtandao ya mwaka 2015, endapo mtuhumiwa atabainika kusambaza picha au
video za ngono au zinazoashiria vitendo vya ngono, adhabu ya kosa hilo
ni pamoja na faini ya shilingi milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka
saba jela au vyote kwa pamoja.
Chanzo- EATV
Comments
Post a Comment