Baada ya kuzungumza na Serikali, makamu
wa Rais wa Benki ya Dunia (WB) Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem amesema
kuna masharti wamekubaliana kabla Tanzania haijapewa mkopo wa Dola 300
milioni za Marekani (Sh680.5 bilioni) kwa ajili ya kuboresha elimu
nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Dk Ghanem alisema benki hiyo inatoa fedha kwa ajili ya wasichana wote
bila kujali hali zao, hivyo kuwatenganisha kwa kigezo cha ujauzito au
kingine chochote ni kwenda kinyume na mkakati wa elimu jumuishi.
“Wataalamu wetu watashirikiana na
Serikali kuona ilivyojiandaa kutoa elimu kwa wasichana wote.
Tutakapojiridhisha bodi ya wakurugenzi itaidhinisha mkopo husika.
Kuchelewa kwake kutategemea lini Serikali itatekeleza masharti
tuliyokubaliana,” alisema.
Mkopo huo ilikuwa ujadiliwe na
kuidhinishwa Oktoba 30, lakini kutokana na msimamo wa Serikali kutotoa
fursa ya kuendelea na masomo wasichana wanaopata mimba, bodi ya benki
hiyo ilisitisha kuujadili. Kwa utaratibu wa benki hiyo, kabla mradi
wowote haujaidhinishiwa fedha zinazohitajika, huujadili kwanza. “Mradi
wa Tanzania haujajadiliwa. Lakini kwa mazungumzo tuliyofanya,
utajadiliwa Serikali itakapotimiza masharti tuliyokubaliana,” alisema Dk
Ghanem.
Baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu
jijini Dar es Salaam juzi, Rais John Magufuli alisema benki imekubali
kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara,
nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia.
“Kwa hiyo, (Dk Hafez) amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha,” alisema Rais Magufuli.
Vilevile, Dk Ghanem alisema
walizungumzia mabadiliko ya Sheria ya Takwimu na wameishauri Serikali
kuhakikisha wadau wake wanakuwa huru kukusanya na kutumia takwimu.
Alisema WB haiwezi kufanyakazi bila
takwimu ambazo zitakusanywa kwa uhuru, lakini masharti yaliyomo kwenye
muswada, huenda yakazorotesha ufanisi wake.
Comments
Post a Comment