RC MTAKA: HATUJAWAKATAA WADAU WA AFYA TUNATAMBUA MCHANGO WAO, TUNAOMBA WAZINGATIE VIPAUMBELE VYA KITAIFA
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony
Mtaka akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake Machi
O2, 2018 Mjini Bariadi.
|
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali Mkoani humo haijawakataa wadau wa Afya
kutoka katika Mashirika mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa wanaofanya kazi
mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye Sekta
ya Afya , bali inatambua mchango wao na inawaomba kufanya kazi kwa kuzingatia
vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa kwenye Sekta ya Afya.
Mtaka ameyasema hayo katika
mazungumzo maalum na waandishi wa Habari wakati alipokuwa akifafanua kauli
aliyoitoa katika kikao kilichofanyika Februari 25 na 26 Mjini Bariadi kati ya
Viongozi wa Mkoa huo na Wadau Afya mkoani humo ya kuwataka kuelekeza zaidi
fedha zao katika kujibu mahitaji ya wananchi kwenye Afya badala ya semina na mafunzo
kwa watumishi.
Amesema
Serikali inatambua mchango wa Mashirika na wadau wa Afya Mkoani humo kutokana
na mambo waliyoyafanya kuunga mkono Serikali kutatatua changamoto mbalimbali za
Sekta ya Afya, ikiwa ni pamoja na kutoa magari, kujenga majengo ya upasuaji katika
baadhi ya Vituo vya Afya na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.
Ameongeza
kuwa pamoja na michango hiyo Mashirika mengi yanayofanya kazi Mkoani Simiyu
katika Sekta ya Afya yameonekana kujikita zaidi katika kutoa fedha nyingi kwa
ajili ya semina na mafunzo kwa watumishi wa Afya , badala ya kusaidia katika
kutatua changamoto ambazo ni vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa pia katika Sekta ya
Afya.
Aidha,Mtaka
amebainisha kuwa Vipaumbele vya Kitaifa na Mkoa katika Sekta ya Afya ni pamoja na Ujenzi wa Miundombinu
ya Afya ambayo ni majengo ya zahanati, vituo vya afya, vyumba vya upasuaji,
hospitali), Vifaa pamoja na vifaa tiba, ambapo alieleza kuwa Mkoa huo una upungufu wa
Hospitali ya Mkoa, Hospitali mbili za Wilaya, Vituo vya Afya 112 na Zahanati
291.
“Tumepitia
bajeti za mashirika haya 11 kwa ujumla wake mwaka 2018 yatatumia zaidi ya
shilingi bilioni 21, hizi ni fedha nyingi ambazo kama zitafanya kazi
inayoonekana huduma za Afya ndani ya mkoa zitaimarika, changamoto kubwa ambayo
mimi kama mkuu wa mkoa na viongozi wenzangu tumeiona ni fedha nyingi kati ya
hizo kuelekezwa kwenye mafunzo ya watumishi wa afya” alisema
“Kwanza
nimeyaomba mashirika yanayofanya kazi za Sekta ya Afya ndani ya Mkoa kila moja kuonesha kazi wanazofanya, pili
natoa wito kwa mashirika haya kuelekeza fedha nyingi kwenye kuongeza idadi ya
vituo vya afya, zahanati, vifaa na vifaa tiba ili tunapojenga uwezo kwa
watumishi wetu wa Afya wawe na mahali pa kwenda kufanyia kazi mafunzo
wanayopata” alisisitiza Mtaka
Ameongeza
kuwa Ofisi yake imeandika barua Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili Viongozi kutoka Wizara hizo mbili
wakutanishwe pamoja na Viongozi wa Wizara ya Afya na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu
kwa lengo la kujadili na kuchambua tija ya fedha za wadau/mashirika hayo kwenye
Sekta ya Afya.
Mmoja
wa wadau hao Mwakilishi kutoka Shirika
la Mkapa Foundation Bi.Adeline Saguti akichangia hoja katika kikao chao na
Viongozi wa Mkoa wa Simiyu alisema Wadau wa Afya Mkoani humo wameahidi
kushirikiana na Mkoa huo kufanyia kazi
maeneo yenye uhitaji katika Sekta ya Afya.
Wadau
wa Afya (mashirika ya ndani na nje ya nchi) wanaofanya kazi na mkoa wa Simiyu
ni pamoja na AMREF, AGPAHI, CUAMM, UNFPA, Mkapa Foundation, AMERICARE, Red
Cross, ICAP, TAMA, INTRAHELTH, WORD VISION na BORESHA AFYA.
Comments
Post a Comment