Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amelitaka
Shirika la Maji Safi na Maji Taka DAWASCO kuhakikisha linashughulikia
kero zote za maji kwa Wananchi ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa maji
safi na kupatia ufumbuzi tatizo la Maji Taka yanayotiririka holela
kwenye makazi ya watu.
RC Makonda ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya
Maji ambapo amesema tatizo la maji taka limekuwa kero sugu katika maeneo
mbalimbali ya jiji hilo jambo linalohatarisha hata Afya za wananchi.
Aidha RC Makonda ameitaka DAWASCO kuongeza jitihada za
kufikisha huduma ya maji kwa wananchi ili kuenda sambamba na sera ya
Serikali ya awamu ya Tano ya kumtua mama ndoo kichwani.
Hata hivyo RC Makonda ametoa wito kwa watumishi wa DAWASCO
wanaokwenda kusoma mita kwa wananchi kuwa na lugha nzuri kwa wananchi
pamoja na kushughulikia kero ya wananchi kubambikiziwa kiwango kikubwa
cha malipo ya bili za maji.
Kuhusu changamoto ya upotevu wa maji RC Makonda amelitaka
shirika hilo kulipatia majibu ya haraka tatizo hilo ili kiasi cha maji
yanayopotea kiweze kuwahudumia wananchi.
Ili kufikisha huduma ya maji kwa maeneo yenye changamoto RC
Makonda amejitolea kuchimba visima 50 vya maji ambapo amewasihi
Wenyeviti wa mitaa hiyo kuainisha maeneo ya kuchimba visima hivyo.
Pamoja na hayo RC Makonda ametaka uwepo wa ushirikiano wa
kikazi baina ya TANROAD, TANESCO, TARURA na DAWASCO ili kumaliza
changamoto ya kukatwa kwa miundombinu ya maji wakati wa ujenzi wa
barabara pamoja na uharibifu wa barabara.
Comments
Post a Comment