Naibu Waziri wa Madini Doto
Biteko ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya madini nchini, kuzingatia sheria
mpya ya madini ambayo inaelekeza namna bora ya usimamizi wa sekta hiyo.
Alitoa wito huo jana, Machi 22
mwaka huu kwa nyakati tofauti, alipokuwa katika ziara ya Mkoa wa Dodoma,
kukagua shughuli mbalimbali za madini.
“Moja ya mambo muhimu ambayo
sheria mpya ya madini inaelekeza ni kutunza rekodi za uzalishaji wa madini ili
Serikali iweze kujua ni kitu gani kinazalishwa na hatimaye tuweze kujua kodi
gani zinalipwa na wenye leseni husika,” alifafanua.
Aidha, Naibu Waziri aliwataka
wenye leseni kushirikiana na wachimbaji wadogo wa madini ili waweze kunufaika
kupitia kazi wanazofanya. “Kwa maneno mengine, asitokee mtu wa kumnyanyasa
mchimbaji mdogo eti kwa sababu tu ana leseni,” alisisitiza.
Akizungumza na wamiliki wa
leseni pamoja na wachimbaji wadogo wa madini wa dhahabu katika eneo la Nholi
wilayani Bahi, Naibu Waziri alipongeza uamuzi wao wa kuanzisha kampeni ifikapo
Aprili mwaka huu, kupanda miti kwenye maeneo yao ili kurejesha hali nzuri ya
mazingira.
Vilevile, aliwaagiza kuweka
wigo kuzunguka mashimo yaliyo wazi ili kuonyesha hali ya tahadhari kuwa eneo
hilo ni hatari na linaweza kusababisha ajali, ikiwa ni hatua mojawapo ya
kuzingatia usalama migodini.
Akizungumzia changamoto kuu
iliyowasilishwa kwake na wachimbaji wa mawe ya nakshi aina ya Granite na
Dorelite Dyke katika maeneo ya Itiso wilayani Chamwino na Ntyuka Wilaya ya
Dodoma Mjini, kuhusu vibali vya kusafirisha mawe hayo nje ya nchi,
Biteko
alisema kuwa awali Serikali ilisimamisha utoaji vibali hivyo kuzuia
usafirishaji wa mawe ghafi nje ya nchi.
“Changamoto iliyokuwepo awali,
ni kuwa wako watu walikuwa wanasafirisha madini nje ya nchi yakiwa ghafi,
yanaongezwa thamani huko kasha tunarejeshewa sisi tununue bidhaa hizo.”
Akifafanua zaidi, alisema kuwa,
jambo linalotia moyo ni kwamba uongezaji thamani madini hivi sasa umeanza
kufanyika nchini kwa kiwango kinachotakiwa kusafirishwa nje ya nchi. Alisema,
jambo hilo hilo litaleta manufaa kwani thamani, ajira na teknolojia vyote
vitabaki ndani na manufaa yatabaki ndani ya nchi pia.
Alipongeza wachimbaji wa mawe
ya nakshi wa Itiso na Ntyuka ya kudhamiria kujenga mitambo ya uongezaji thamani
mawe hayo katika maeneo husika.
Alisema kiu ya Serikali ni
kuona madini yanayochimbwa Tanzania, yanaongezwa thamani nchini na hatimaye
kusafirisha bidhaa zinazotokana na madini hayo na kuziuza katika nchi nyingine
mbalimbali na siyo vinginevyo.
Aidha, Naibu Waziri
aliwasisitiza wamiliki wote wa leseni za madini kufanya kazi zao huku
wakizingatia kujenga mahusiano mema na jamii zinazowazunguka.
Alisema kuwa kmujibu wa kanuni
mpya iliyopo hivi sasa, mwenye leseni anapaswa kuwasilisha mpango wake wa
utoaji huduma kwa jamii (CSR) kwenye Halmashauri husika ili iuthibitishe mpango
huo kabla ya utekelezaji wake.
“Ule utaratibu wa mtu
anajifungia ofisini, anasema nitawajengea shule pasipo Serikali ya Kijiji au
Wilaya kujua, tumeufuta kwa sababu mwanzo ulikuwa unatengeneza matatizo mengi,”
alifafanua Biteko.
Alisema, Serikali itafanya kazi
ya kuangalia na kuthibitisha thamani halisi ya fedha zitakazotumika katika
mpango huo, ili kujiridhisha.
Naibu
Waziri alimwagiza Afisa Madini Mkazi wa Dodoma Silimu Mtigile kuandaa na
kuendesha semina siku ya Jumatatu, Machi 26 mwaka huu, kwa ajili ya wachimbaji
wa eneo la Nholi kuhusu sheria mpya ya madini, kufuatia maombi waliyowasilisha
kwake alipokuwa akizungumza nao.
Hata hivyo, alisema kuwa semina
za aina hiyo zitaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini kote ili
kuwajengea uelewa wa sheria hiyo mpya wadau wa madini waweze kufahamu haki na
wajibu wao.
Akizungumzia suala la baadhi ya
watu kueneza propaganda kuhusu sheria hiyo kuwa ni kandamizi; Biteko aliwataka
watanzania kupuuza kauli hizo kwani sheria husika imelenga kuwanufaisha
watanzania na siyo kinyume chake.
“Kama kuna bepari anadhani
kwamba tunaweza kurudi nyuma katika hili, amekwama. Heri tuwe na wawekezaji
wachache wanaofuata sheria kuliko kuwa nao wengi wenye kutaka tu kuchuma mali
na kuondoka.”
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri
Biteko aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Dodoma Silimu Mtigile, wataalam
kutoka wizarani na ofisi ya madini Dodoma pamoja na viongozi wa Wilaya na
Halmashauri akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Elizabeth Kitundu.
Comments
Post a Comment