Watuhumiwa wakipelekwa kupanda gari la polisi kwa ajili yakuwapeleka rumande
Kaimu Meneja wa Mamcu bwana Kelvin Rajabu akipanda gari la polisi tayari kwakwenda rumande.Picha na Chris Mfinanga
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akimuhoji Kaimu Meneja mkuu wa chama kikuu cha
ushirika Masasi Mtwara (MAMCU) Bwana Kelvin Rajabu kuhusiana na upotevu
wa koroshozaidi ya tani 2000 Waziri mkuu alifanya kikao na Bodi ya
korosho pamoja na baadhi ya wanaushirika Mamcu kikao hicho kimefanyika
katika ukumbi wa mikutano Ikulu ndogo Mkoani Ruvuma
Kamanda
wa polisi mkoani Ruvuma Zuberi Mwombeji akiwatarifu Maofisa wa Mamcu na
Yurap wako chini ya ulinzi wa polisi kuhusiana na upotevu wa korosho
tani 2000 kulia mwenye kaunda suti Kaimu meneja mamcu Bwana Kelvin
Rajabu anayefuatia Mkurugenzi wa YURAP inayojishughulisha nauhifadhi
korosho katika Ghala la BUCO Masasi Bwana Yusuf Namkula anayefuatia
Mkurugenzi mwenzake Bwana Ramadhan Nama na Meneja tawi la Mamcu Bwana
Lawrence Njozi
*Ni kwa tuhuma za uzembe na upotevu korosho zaidi ya tani 2,000
* Wapelekwa Masasi chini ya ulinzi wakajibu tuhuma zinazowakabili
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma,
Kamishna Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na
kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za
upotevu wa tani 2, 138 za korosho.
Maafisa
hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU),
Bw. Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi. Wengine ni
wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa
mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.
Waziri
Mkuu alifikia uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini jana
jioni (Jumamosi, Januari 7, 2017) baina ya watendaji kutoka Bodi ya
Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO – Masasi na kikundi
cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi
(AMCOS) za wilaya za Mtwara na Masasi.
Katika
kikao hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo
hizo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana
inaonyesha kuwa waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo
haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.
Kaimu
Meneja Mkuu wa MAMCU, Bw. Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu
kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa an wanunuzi wa mnda wa tano
lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha
korosho. Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Bw. Ramadhan Namakweto alikiri
kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa
maelezo ni kwa nini hazionekani zilipo.
“Tangu
mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada
wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho za hawa
wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku
taarifa yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri
Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.
Tuhuma
zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile
zilizowasilishwa ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na
kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo. Mfano ni kufanya makato ya
unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya
Serikali.
Nyingine
ni kutowalipa fedha kwa wakati wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa
tano wa tarehe 10 Novemba 2016 na kutokutoa maelezo yoyote licha ya
kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na kupokea
malipo.Nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za
korosho zilizokuwa katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11,
mwka jana; kutokutolewa taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka
husika na kuwasababishia hasara wananchi.
Tuhuma
nyingine ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya tani 1,156,262
ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016. Korosho
hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga
Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani
(229,189).
Kutokana
na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza watu hao wapelekwe Masasi chini
ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na
kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na
kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya
msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada
husika.
Mapema,
wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima hao walisema wana kero
nyingi sana kama vile kutolipwa fedha zao kwa wakati; kutoeleweka mahali
zilipo korosho ambazo walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu
ambayo Serikali ilikwishapiga marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao
na viongozi wa MAMCU pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya.
“Makubaliano
yalikuwa ni kwamba mkulima atapewa fedha yake siku sita baada ya mnada
kufanyika lakini hivi sasa baadhi yetu tumeuza korosho tangu Oktoba,
mwaka jana lakini hadi imefika Januari hii bado hatujalipwa. Pia kuna
makato yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu lakini wao
wameyaacha na unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia
gharama za unyaufu,” alisema msoma risala Bw. Sylvester Mtimbe ambaye
pia ni mkulima kutoka AMCOS ya Chiungutwa.
Wakulima
hao wa korosho kutoka Masasi mkoani Mtwara walikutana Januari 3, 2017
katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa wangeandamana hadi Dar es
Salaam ili wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au kwa Mheshimiwa Rais
Dk. John Magufuli.
Kwa
kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar es Salaam na kwamba yeye
hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu aliamua
kuwaita wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi
ya siku nne.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JANUARI 8, 2017.
Comments
Post a Comment