WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Idara kwenye Halmashauri za
Wilaya na Manispaa wasaidie kutoa utaalamu badala ya kupingana na
madiwani ili wawezeshe kuleta maendeleo kwa wananchi.Pia amewataka
madiwani wasikilize ushauri wa kitaalamu unaotolewa na Wakuu wa Idara
katika utekelezaji wa miradi iliyotengwa na Halmashauri.
Ametoa
wito huo leo mchana (Alhamisi, Januari 5, 2017) wakati akizungumza na
watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mabada na viongozi na
watendaji wa mkoa wa Ruvuma akiwa katika siku ya pili ya ziara yake
mkoani humo.
“Wakuu wa
Idara nyie ni washauri. Tumieni taaluma zenu kutoa ushauri, semeni bila
woga pale inapodidi. Ninawasihi waheshimiwa madiwani wasitumie fursa
yao ya ‘kuazimia’ pale inapotokea kuna watumishi wenye msimamo,”
amesema.
Akizungumzia
kuhsu ukusanyaji wa mapato, Waziri Mkuu amesema Serikali iko makini
kwenye matumizi kwa kila senti inayokusanywa na akawataka watumishi hao
kila mmoja aongeze mapato ya Serikali kupitia sekta aliyopo. Pia amepiga
marufuku matumizi holela ya fedha za umma.
“Kuanzia
leo, marufuku kwa fedha iliyokusanya kwa mapato ya ndani kutumika bila
utaratibu. Serikali hii haina mzaha na miradi inayotekelezwa chini ya
viwango. Mtumishi ukiharibu hapa Madaba, usidhani utahamishwa,
tunamalizana na wewe hapahapa. Wala usiombe ndugu yako akuombee
uhamisho, tutakufuata hukohuko,” amesisitiza.
Amewataka
watumishi wa umma wote watumie Ilani ya Chaguzi ya CCM katika
kutekeleza majukumu kwani inaeleza kila kitu ambacho Serikali inatakiwa
kukifanya katika kipindi ca miaka mitano.
“Zaidi ya
hayo, ninawasihi kila Mkurugenzi atoe nakala ya hotuba ya Mheshimiwa
Rais ambayo aliitoa Novemba 20, 2015 wakati akizindua Bunge la 11, awape
watendaji wake waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha
kwani ilitoa dira ya nini anataka kufanya katika Serikali hii,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema Serikali kwa upande wake inaendelea kuboresha maslahi ya
watumishi na imeanza kulipa madeni yaliyokuwa yamelimbikizwa. “Serikali
imedhamiria kupunguza madeni ya watumishi na hadi kufikia Novemba 30,
2015 jumala ya sh. bilioni 28.9 zilikuwa zimekwishlipwa kwa watumishi
31,032 wenye madai katika sekta mbalimbali. Zoezi hili linaendelea.”
Alitumia
fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa wilaya hiyo wajibu wao wa
kuwahudumia Watanzania bila kujali dini, itikadi, kabila au hali zao na
akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza
wajibu wake.
Akifafanua
kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu amesema Serikali
imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri
kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.
"Hii
imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili
imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa
za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti
kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine
alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo, " amesema.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JANUARI 5, 2017.
Comments
Post a Comment