Hillary
Clinton na mumewe Bill wamethibitisha kwamba watahudhuria sherehe ya
kuapishwa kwa rais mpya wa Marekani Donald Trump mjini Washington DC.
George W
Bush na mkewe Laura pia wametangaza kwamba wanapanga kuhudhuria sherehe
hiyo mnamo tarehe 20 Januari. Wamesema wanataka "kushuhudia kukabidhiwa
madaraka kwa rasi mwingine kwa njia ya amani."
Tajiri
huyo kutoka Manhattan, New York ataapishwa kuwa rais wa 45 wa Marekani
katika makao makuu ya serikali Capitol Hill. Bw Trump alimshinda Bi
Clinton katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba mwaka jana na amemkosoa
Bw Bush kutokana na vita vya Iraq na mashambulio ya 9/11.
Kabla ya
tangazo hilo la Jumanne, Jimmy Carter alikuwa ndiye rais wa zamani pekee
aliyekuwa amesema angehudhuria sherehe hiyo. Rais mwingine mstaafu
George HW Bush, 92, amesema hataweza kuhudhuria kutokana na umri wake.
Bi
Clinton amekuwa haonekani sana hadharani tangu aliposhindwa na Bw Trump
uchaguzini Novemba. Wakati wa kampeni, Bw Trump alimweleza kama mtu
mwovu na asiye wa kuaminika.
Bw Trump
pia amekosoa madai ya George W Bush kwamba alihakikisha Wamarekani
walikuwa salama zaidi wakati wa utawala wake. Alisema shambulio la
Septemba 11 mwaka 2001 (9/11) lilitekelezwa wakati wa utawala wake.Aidha,
amemshutumu rais huyo wa 43 kwa kusema uongo kuhusu kuwepo kwa silaha
za maangamizi makubwa nchini Iraq. Bw Trump alishambulia pia mtu
mwingine wa familia ya Bush, gavana ya Florida Jeb Bush ambaye alikuwa
anakabiliana naye kwenye mchujo chama cha Republican na kumtaja kama
"aliyepungukiwa na nguvu".
Chanzo: BBC Swahili
Comments
Post a Comment